Dec 07, 2019 02:46 UTC
  • Ugiriki yamtimua balozi wa Libya kulalamikia hati ya maelewano iliyosainiwa kati ya Libya na Uturuki

Serikali ya Ugiriki imemtimua balozi wa Libya mjini Athens, kufuatia kutiwa saini hati ya maelewano ya ushirikiano wa baharini kati ya Uturuki na serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya.

Nikos Dendias, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki aliwaambia waandishi wa habari jana Ijumaa kwamba kutiwa saini hati ya maelewano ya ushirikiano wa baharini kati ya serikali za Ankara na Tripoli, ni ukiukaji wa wazi wa sheria na mikataba ya kimataifa na kufuatia hali hiyo serikali ya Athens imempa muda wa saa 72 balozi wa Libya nchini humo awe ameondoka ardhi ya Ugiriki. Kadhalika Dendias amebainisha kwamba kumuondoa balozi huyo wa Libya nchini humo, hakumaanishi kukatwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Athens na Tripoli, na kuongeza kuwa uamuzi huo umechukuliwa baada ya upande wa Libya kukataa masharti yaliyotolewa na Ugiriki kuhusiana na kadhia hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki, Nikos Dendias

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki amesema kuwa Mohamed Taher Siala, Waziri wa Mambo ya Nje ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya alikuwa na uwezo wa kuzuia kutiwa saini hati hiyo ya maelewano. Uturuki na Libya zilisaini hati hiyo tarehe 27 Novemba mwaka huu mjini Istanbul, Uturuki kwa kuhudhuriwa na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa nchi hiyo pamoja na Fayez al-Sarraj, Rais wa serikali ya umoja wa kitaifa inayotambuliwa na jamii ya kimataifa, mapatano ambayo yanaainisha maeneo ya upenyaji wa baharini kati ya nchi hizo na kuimarisha ushirikiano wa kiusalama wa pande mbili. Nchi za Misri na Cyprus pia zimetoa taarifa ya pamoja kwa kuungana na Ugiriki ambapo zimepinga makubaliano hayo kati ya Uturuki na Libya kuhusiana na maeneo ya baharini.

Tags

Maoni