Dec 07, 2019 12:09 UTC
  • Sisitizo la Araqchi juu ya udharura wa kutekelezwa majukumu ya pande zote ndani ya JCPOA

Kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya Makubaliano ya Nyukilia ya JCOA katika ngazi ya Manaibu na Wakurugenzi Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje za Iran na nchi wananchama wa kundi la (4+1) linaloundwa na Ujerumani, Ufaransa, Russia, China na Uingereza kilifanyika jana Ijumaa mjini Vienna Austria.

Kama kawaida, kikao hicho kilipangwa kufanyika katika hoteli ya Coburg huko Vienna hata hivyo kwa kuzingatia kutolewa kibali cha kukusanyika mbele ya hoteli hiyo kundi  la wafuasi wanaotaka kujitenga na walio dhidi ya Mapinduzi; na kuwepo pia uwezekano wa kuvurugwa  kikao hicho cha kamisheni ya pamoja ya JCPOA; ujumbe wa Iran ulilalamikia hatua hiyo na kutishia kuondoka kwenye mazungumzo; ambapo baadaye sehemu ya kufanyika kikao hicho ilibadilishwa na kisha  kikao kikafanyika katika jengo la wawakilishi wa Umoja wa Ulaya huko Vienna.  Kikao hicho kilianza kwa kuchelewa kwa muda wa saa moja. 

Sayyid Abbas Araqchi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa na Bi Helga Schmid Naibu Afisa wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya ndio waliosimamia kikao hicho.  

Kama alivyoashiria Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran mwishoni mwa kikao hicho licha ya kuwepo ukosoaji uliobainishwa na pande mbili katika kikao hicho cha kamisheni ya pamoja ya JCPOA lakini imebainika kuwa wanachama wote wana mtazamo mmoja kuhusu masuala mawili. La kwanza ni kuwa, katika kikao hicho wanachama wote wamethibtisha kuwa Marekani ndio chanzo cha mivutano iliyopo katika makubaliano ya JCPOA. Araqchi amesema baada ya kumalizika kikao cha kamisheni ya pamoja ya JCPOA mbele ya waandishi wa habari kuwa: Wanachama wote wanapinga kushadidishwa vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na wanasisitiza kuwa mapatano hayo kimataifa hayawezi kudumishwa bila ya Iran kunufaika na maslahi yake. 

Mikhail Ulyanov Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Taasisi za Kimataifa zenye makao yake mjini Vienna jana aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: Natija kuu ya mijadala iliyofanyika katika kikao cha leo cha kamisheni ya pamoja ya JCPOA ni mtazamo kamili wa pamoja wa nchi zote wanachama wa makubaliano ya JCPOA kuhusu udharura wa kuyaunga mkono mapatano hayo ya kimataifa na kufungamana nayo.  

Mikhail Ulyanov, Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Taasisi za Kimataifa zenye makao yake mjini Vienna 

Suala jingine lililotiliwa mkazo kwenye kikao hicho ni kuweko mtazamo wa pamoja kuhusu udharura wa kutekeleza makubaliano ya JCPOA na kuyaharakisha ili kupata ufumbuzi wa kuyalinda mapatano hayo. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mei Nane mwaka huu, yaani mwaka mmoja baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja katika makubaliano hayo ya nyuklia na baada ya kuthibitika kushindwa kutekelezwa ahadi za Ulaya kwa ajili ya kudhamini maslahi ya Iran kwa mujibu ya JCPOA, iliamua kusitisha sehemu ya majukumu yake kuhusiana na makubaliano hayo kwa mujibu wa vipengee vya 26 na 36 vya makubaliano hayo. Hata hivyo nchi za Ulaya licha ya kuwa zimeshindwa kuyalinda makubaliano hayo kabla ya kuanza kikao hicho cha Vienna, ziliibua suala la makombora nje ya mjadala  kama kisingizio  cha kukwepa ukosoaji wa Iran kwa hatua yao ya  kushindwa kutekeleza majukumu yao ndani ya makubaliano hayo ya nyuklia.  Uingereza, Ufaransa na Ujerumani Jumatano iliyopita zilimtumia barua Antonio Gutteres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa zikidai kuwa baadhi ya makombora ya balistiki ya Iran hayaambatani na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la umoja huo liliopasisha makubaliano hayo ya nyuklia na Iran. 

Nchi husika katika makubaliano ya nyuklia na Iran baada ya Marekani kujitoa kwenye JCPOA

Madai kwamba makombora ya Iran hayaambatani na azimio la Baraza la Usalama yametolewa katika hali ambayo azimio nambari 2231 la Umoja wa Mataifa liliitaka Iran kutounda makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia. Ulaya iliipatia Iran mapendekezo 11 baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya JCPOA  na kuwasilisha mfumo malumu wa mabadilisho ya kifedha kwa jina la INSTEX kwa ajili ya kudhamini maslahi ya Iran katika makubaliano hayo kama utangulizi wa kutekeleza ahadi zake; mfumo ambao hadi sasa hatima yake haifahamiki.

Bila shaka Iran itaendelea kupunguza ahadi na kuwajibika kwake kwa mujibu wa makubaliano hayo ya nyuklia hadi pale maslahi yake yakapodhaminiwa.  

Tajiriba aidha inaonyesha kuwa kuipa Iran masharti badala ya pande zilizosalia katika makubaliano hayo  kutekeleza ahadia zao hakusaidii kutatua matatizo yaliyopo. Hii ni kwa sababu, tayari Iran imelegeza sana misimamo yake na kuonyesha subira kubwa ya kistratejia katika uwanja huo. 

Hivi sasa tunapasa kusubiri na kuona ni kwa kiwango gani mashauriano ya jana Ijumaa huko Vienna yanaweza kudhamini matarajio katika fursa za mwisho zilizosalia kwa ajili ya kuyalinda makubaliano hayo ya nyuklia.  Awali Araqchi alisema kuwa bado kuna matumaini ya kuyanusuru makubaliano ya nyuklia ya JCPOA; hata hivyo pande za Ulaya ndizo zinazopasa kufungamana na suala hilo la kutekeleza ahadi zao katika makubaliano hayo ya pande kadhaa.  

Maoni