Dec 07, 2019 12:28 UTC
  • Marekani yamuachilia huru mwanasayansi Muirani baada ya kumshikilia kinyume cha sheria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Marekani imemuachilia huru mwanasayansi Muirani Profesa Masoud Suleimani baada ya kumshikilia kwa zaidi ya mwaka mmoja kinyuma cha sheria.

Katika ujumbe alioutuma kupitia ukurasa wake wa Twitter leo Jumamosi, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika: "Nina furaha kutangaza kuwa, Profesa Masoud Suleimani na Bw. Xiyue Wang watajiunga na familia zao hivi karibuni."

Zarif aidha amewashukuru wale wote waliohusika na suala hilo hasa serikali ya Uswisi.

Mwanasayansi Muirani, Profesa Masoud Suleimani, amekuwa akishikiliwa nchini Marekani kwa muda wa mwaka mmoja sasa kinyume cha sheria.

Leo wakuu wa Uswisi wamemkabidhi Profesa Suleimani kwa wakuu wa Iran.

Xiyue Wang, raia wa Marekani mzaliwa wa China, alikuwa anahudumia kifungo cha miaka 10 gerezani nchini Iran baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi. Wang pia amekabidhiwa wakuu wa Uswisi na anatazamiwa kujiunga na familia yake hivi karibuni.

Profesa Masoud Suleimani (wa tatu kutoka kulia) akiwa katika Ubalozi wa Iran nchini Uswisi

Ikumbukwe kuwa mnamo Oktoba 25, 2018, Profesa Suleimani ambaye ni mwanasayansi wa seli shina na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Tarbiat Modares, alifika katika uwanja wa ndege wa Chicago kufuatia mwaliko wa taasisi moja ya utafiti Marekani. Punde baada ya kuwasili Profesa Suleimani alitiwa mbaroni na makachero wa FBI na tokea wakati huo alikuwa katika kizuizi bila kuruhusiwa kuwa na mawasiliano yoyote na jamaa zake.

Wanaharakati wa kijamii walianzisha kampeni ya  kimatiafa inayojulikana kama #Free_Masoud_Soleimani ili kuwashinikiza wakuu wa Marekani wamuachilie huru msomi huyo wa Iran.

Tags

Maoni