Dec 08, 2019 07:12 UTC
  • Wanasheria 500 wa Marekani: Mchakato wa kumuuzulu Trump ni halali kisheria

Wanasheria 500 nchini Marekani wameliandikia barua bunge la nchi hiyo na kueleza kwamba kwa mujibu wa katiba, mwenendo na utendaji wa Rais Donald Trump unaingia kwenye hukumu ya "uhaini" na kwa hiyo anastahili kusailiwa na kuuzuliwa.

Katika barua yao hiyo waliyoiandikia Kongresi ya Marekani hapo jana, mawakili hao wamebainisha kuwa, kuna ushahidi madhubuti unaothibitisha kwamba Trump amesaliti kiapo alichokula cha wadhifa wake wa urais.

Barua ya wanasheria hao 500 wa Marekani imesisitiza kuwa, rais wa nchi hiyo ametumia madaraka yake kuishinikiza serikali ya nchi ya kigeni kwa ajili ya kuathiri mwenendo wa uchaguzi ujao wa Marekani.

Trump kwa sasa amekuwa akiandamwa na kashfa mpya inayojulikana kama "Ukrainegate".

Hivi karibuni 'mripuaji bomu' asiyejulikana alifichua kwamba, katika mazungumzo ya simu aliyofanya Trump mwezi Julai mwaka huu na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, rais huyo wa Marekani alimtaka kiongozi huyo ampatie taarifa zitakazochafua haiba ya Joe Biden, anayewania kuwa mgombea urais wa mwaka 2020 kwa tiketi ya chama cha Democrat na ambaye anaonekana kuwa ndiye mshindani mkuu wa Trump katika kinyang'anyiro hicho.

Donald Trump (kushoto) na Joe Biden

Inasemekana kuwa Trump aliishurutisha Ukraine kufanya uchunguzi kuhusu ufisadi anaodaiwa kufanya Biden na mwanawe wa kiume Hunter Biden ili kuweza kuipatia nchi hiyo msaada wa dola milioni 250 kwa ajili ya masuala ya kijeshi.

Kufuatia kufichuliwa kwa kashfa hiyo, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi alitangaza kuanza mchakato wa kumuuzulu Donald Trump, ambao hadi sasa umeshaungwa mkono na wajumbe wasiopungua 225 wa baraza hilo.

Mnamo tarehe 24 Septemba, Bi Pelosi alitangaza kuwa hakuna mtu yeyote ndani ya Marekani aliye juu ya sheria na kusisitiza kwamba Baraza la Wawakilishi linaanzisha rasmi uchunguzi kuhusiana na kumuuzulu Trump.

Wademokrati wanaitakidi kuwa hatua ambazo rais wa nchi hiyo amezichukua hadi sasa zimekiuka kwa uwazi kabisa katiba ya Marekani.../

 

Maoni