Dec 08, 2019 07:13 UTC
  • Saudia yatakiwa izilipe fidia familia za waathiriwa wa shambulio la kigaidi la Florida

Gavana la jimbo la Florida nchini Marekani ameitaka Saudi Arabia izilipe fidia familia za watu waliouliwa katika shambulio la kigaidi, lililolenga kituo cha kijeshi cha Pensacola kilichoko katika jimbo hilo.

Kanali ya televisheni ya Al-Alam imemnukuu gavana wa jimbo hilo Ron DeSantis akisema: Saudi Arabia ina deni kwa Marekani na waathiriwa wa ufyatuaji risasi uliofanywa kwenye kituo cha kijeshi cha jimbo hili; na inapaswa ilipe deni hili.

Mohammed Saeed Alshamrani, raia wa Saudia, ambaye alikuwa nchini Marekani kwa ajili ya mafunzo ya urubani, siku ya Ijumaa aliwapiga risasi na kuwaua watu watatu katika shambulio alilofanya dhidi ya kituo cha anga cha Jeshi la Wanamaji la Marekani kilichoko Pensacola, jimboni Florida.

Kabla ya kufanya shambulio hilo la kigaidi, Alshamrani aliandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter: "Ninapinga uovu; na Marekani kwa ujumla imegeuka kuwa taifa la uovu."

Mohammed Saeed Alshamrani

Itakumbukwa kuwa shambulio la kigaidi la Septemba 11, 2001 lilipelekea kujitokeza hisia kali za chuki dhidi ya Saudi Arabia ndani ya Marekani, lakini kwa sababu ya kuhitajia mno mafuta na fedha za Saudia, wanasiasa wa Marekani waliamua kufumbia macho fikra na itikadi zinazochochea na kuhamasisha ugaidi za utawala wa Aal Saud.

Hivi sasa maafisa wa polisi ya Marekani imewatia nguvuni raia sita wa Saudia, katika upelelezi wanaoendelea kufanya kuhusiana na shambulio la ufyatuaji risasi katika kituo cha jeshi jimboni Florida.

Watatu kati ya watu hao waliokamatwa, wanatuhumiwa kuwa walikuwa wakichukua filamu wakati raia mwenzao huyo wa Saudi Arabia alipokuwa akifanya shambulio hilo.../

Maoni