Dec 09, 2019 03:28 UTC
  • Guardian: Marekani, Israel na Uingereza zinahujumu Uislamu kupitia mitandao ya kijamii

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Guardian la Uingereza umebaini kuwa, makundi yenye misimamo mikali yanayofadhiliwa na kuungwa mkono na Marekani, Israel na Uingereza yanadhibiti mitandao ya kijamii ambayo zinaitumia kwa ajili ya kueneza chuki na uhasama dhidi ya Waislamu.

Uchunguzi huo wa gazeti la Guardian umesema kuwa, mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter inazuia na kufunga kurasa zinazoandika habari za kuwaunga mkono Wapalestina au kupinga jinai na uhalifu unaofanywa na Israel. 

Ripoti ya gazeti hilo la Uingereza imesema kuwa: Kurasa za mitandao hiyo zinazowaunga mkono wanamapambano wa Lebanon dhidi ya Israel pia zinafungwa na kuzuiwa. Hivi karibuni pia Facebook ilifunga kurasa za watumiaji wake ambazo zinatoa mitazamo inayotafautiana na siasa za ikulu ya Rais wa Marekani, White House.

Ripoti hiyo imesema makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia ambayo mengi yanafanya harakati katika nchi za Marekani na Uingereza, yamekuwa yakisambaza jumbe zinazochochea chuki na uadui dhidi ya Waislamu na wahajiri wa Kiislamu katika nchi za Ulaya.

Wanachama wa makundi hayo pia wanasambaza habari na ripoti zinazochafua sura ya wanasiasa Waislamu kama Meya wa London Sadiq Khan, Wabunge Waislamu wa Kongresi ya Marekani Ilhan Omar na Rashida Tlaib na vilevile kiongozi wa chama cha Leba cha Uingereza Jeremy Corbyn. 

Ilhan Omar na Rashida Tlaib

Gazeti la Guardian limesisitiza kuwa limewajulisha wakurugenzi wa mtandao wa kijamii wa Facebook kuhusu njama na mtandao huo wa siri unaoeneza chuki dhidi ya Waislamu lakini hawajachukua hatua yoyote.  

Maoni