Dec 10, 2019 02:53 UTC
  • Onyo kali la Russia juu ya kuharibika uhusiano wa nchi hiyo na Shirika la Kijeshi la NATO

Katika miaka ya hivi karibuni uhusiano wa Russia na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) hususan baada ya kuzuka mgogoro wa Ukraine mwaka 2014, umekuwa ni wa mzozo ambapo kiwango cha migogoro na makabiliano baina ya pande hizo mbili kimeendelea kukua mwaka baada ya mwaka.

Hali hiyo imewafanya viongozi wa ngazi ya juu wa kijeshi nchini Russia kutoa indhari kali kuhusiana na suala hilo. Sergey Shoygu, Waziri wa Ulinzi wa Russia amenukuliwa akisema kuwa nchi yake imejiweka tayari kwa ajili ya kushirikiana na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO), lakini wakati huo huo akasisitiza kwamba, uhusiano wa pande mbili unazidi kuwa mbaya mwaka baada ya mwaka. Shoygu amesema: "Uhusiano wa Russia na NATO umezidi kuwa mbaya kila mwaka sambamba na kusimama ushirikiano wa pande mbili. Miaka ya nyuma tulikuwa na uhusiano mzuri na Brussels ambapo Russia pia ilikuwa na mwakilishi wake ndani ya NATO, lakini hii leo washirika hao wakisaidiana na Marekani wamevunja mikataba na kujiondoa katika makubaliano mengi kama ambavyo milango ya usalama imezidi kufungwa." Waziri wa Ulinzi wa Russia ametoa matamshi hayo katika hali ambayo ni siku chache tu zimepita viongozi wa nchi wanachama wa NATO kukutana mjini London, Uingereza. Amefafanua zaidi kwa kusema, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Moscow imejitahidi sana kufuatilia uhusiano mwema na upande wa pili yaani nchi wanachama wa NATO, lakinni uhusiano huo haukuwa na maendeleo mazuri. Kabla ya hapo pia Rais Vladmir Putin wa Russia sambamba na kufanyika mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa NATO mjini London, aliashiria matatizo yaliyopo kati ya nchi yake na muungano huo kwa kusema kuwa, Moscow iko tayari wakati wote kupanua wigo wa ushirikiano wake na NATO. Akizungumzia suala hilo Putin alisema: "Licha ya miamala isiyo ya kuridhisha ya NATO dhidi ya Moscow, kwa mara kadhaa Russia imekuwa ikisisitizia azma na utayarifu wake kwa ajili ya kushirikiana na NATO kwa lengo la kukabiliana na vitisho halisi vya ugaidi wa kimataifa."

Viongozi wa nchi za NATO walipokutana hivi karibuni mjini London, Uingereza

Itakumbukwa kuwa baada ya kuzuka mzozo wa Ukraine na kuongezeka migogoro mingine kati ya Russia na nchi wanachama wa muungano huo huko upande wa Ulaya Mashariki, pande hizo ziliharakisha mwenendo wao wa kuweka upya vikosi vyao vya kijeshi hususan katika vituo viwili vya Bahari ya Baltic na Bahari Nyeusi, suala ambalo halikuwahi kushuhudiwa hapo kabla. Suala lingine ni kwamba ni karibu miongo miwili sasa ambapo Russia imekuwa na daghadagha ya kiusalama kutokana na juhudi endelevu za shirika hilo la kijeshi la NATO za kusonga mbele upande wa mashariki, kuziunga na muungano huo, nchi za Ulaya ya Kati na Mashariki, nchi za ukanda wa Bahari ya Baltic na hatimaye nchi majirani na Russia kama vile Ukraine na Georgia. Russia inatambua ustawi wa shirika hilo upande wa mashariki kuwa ni tishio dhidi ya usalama wake wa kitaifa hivyo mwenendo wa NATO wa kupanua wigo wa wanachama wake ni sababu ya kushtadi mizozo zaidi. Lengo kuu la hatua hizo ni kuifuta na kuidhoofisha zaidi Russia sambamba na kuiwekea mashinikizo zaidi ya kisiasa na kijeshi suala ambalo linapingwa vikali na Moscow. Wakati huo huo kila mwaka suala jipya huzaliwa juu ya masuala ya huko nyuma sambamba na kushadidishwa makabiliano kati ya pande mbili. Kwa upande mwingine ni kwamba taarifa ya mwisho ya kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa NATO mjini London na hatua yao ya kuinyooshea kidole cha lawama Russia, imeisababishia wasi wasi mkubwa serikali ya Moscow kuhusiana na hatua za uhasama za muungano huo wa kijeshi wa nchi za Magharibi. Taarifa hiyo iliwekwa wazi kwamba hatua za kihujuma za Russia ni tishio kwa usalama wa nchi za Ulaya na Amerika Kaskazini na kwa upande mwingine muungano huo ulisisitizia azma yake ya kuweka makombora ya masafa mafupi barani Ulaya kwa ajili ya kukabiliana na Moscow.

Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO)

Aidha taarifa hiyo iliongeza kwamba iwapo Russia itatekeleza hatua chanya, basi NATO itakubali kuwa na uhusiano chanya na nchi hiyo. Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) amesema: "NATO ina imani ya kufanya mazungumzo na Russia na tunaamini kwamba ni lazima tupige hatua itakayotukurubisha zaidi kwa Moscow." Licha ya taarifa ya mwisho ya kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa NATO mjini London, lakini bado viongozi wa muungano huo wa kijeshi wameendelea kuwa na tofauti za mitazamo kuhusu Russia. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki, ambao nchi zao zinahesabiwa kuwa zenye nafasi athirifu katika muungano wa NATO walipinga suala hilo huku wakiutaja ugaidi kuwa ndio tishio kuu la NATO na si Russia. Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Macron alisema: "Russia si adui tena. Hata kama nchi hiyo bado ni tishio lakini kuna baadhi ya mambo bado yanaifanya Moscow kuwa mshirika mkubwa wa nchi za Ulaya. Alisema: Adui yetu hii leo ni ugaidi wa kimataifa; si Russia....." 

Tags

Maoni