Dec 10, 2019 03:20 UTC
  • Luxembourg yaiandikia barua EU kuhusu kutambuliwa rasmi taifa la Palestina

Luxembourg imeuandikia barua Umoja wa Ulaya, ikiutaka umoja huo uitambue rasmi nchi huru ya Palestina.

Jean Asselborn, Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxembourg amemuandikia barua Mkuu mpya wa Sera za Nje wa EU, Josep Borrell, pamoja na mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo, ambapo amesisitiza kuwa, "Kutambuliwa rasmi nchi huru ya Palestina si kuwa ni jambo la fadhila au hundi tupu, bali ni haki halali ya raia wa Palestina kwa ajili ya kuwa na nchi yao."

Katika barua hiyo kwa maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Ulaya, Waziri wa Mambo ya Nje wa Luxembourg ameeleza bayana kuwa, hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuendelea kujenga vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Wapalestina unazozikaliwa kwa mabavu unaweka hatarini mchakato wa amani, mbali na kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Masuala hayo yaliyoashiriwa na Luxembourg katika barua yake kwa Umoja wa Ulaya yanatazamiwa kujadiliwa katika mkutano ujao wa Baraza la Mawaziri wa Mambo wa Nje wa EU Januari mwakani.

Mkuu mpya wa Sera za Nje wa EU aliyechukua mahala pa Federica Mogherini

Wakati huohuo, Miro Cerar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Slovenia amesema nchi wanachama wa EU hazipaswi kufumbia macho 'matukio hatari' yanayofanyika huko Palestina, akisisitiza kuwa anataraji uongozi mpya wa EU utapinga vitendo vya dhulma wanavyofanyiwa Wapalestina.

Mwezi uliopita wa Novemba, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alitangaza kubadilika siasa za Washington kuhusiana na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaofanywa na utawala haramu wa Kizayuni na kudai kwamba kuanzia sasa Marekani haitambui ujenzi huo wa vitongoji kuwa unakiuka sheria za kimataifa.

 

Tags

Maoni