Dec 10, 2019 12:37 UTC
  • Recep Tayyip Erdoğan
    Recep Tayyip Erdoğan

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa, Ankara iko tayari kutuma majeshi nchini Libya iwapo serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo itaomba msaada huo.

Erdoğan amesema kuwa, atafanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Russia kuhusiana na kadhia ya misaada ya kijeshi kwa Jenerali mstaafu Khalifa Haftar ambaye wapiganaji wake wanaendelea kushambulia mji mkuu wa Libya, Tlipoli.

Kuhusiana na makubaliano yaliyotiwa saini siku chache zilizopita baina ya Uturuki na serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya, Rais wa Uturuki amesema nchi yake imetumia haki yake inayotambuliwa rasmi na sheria za kimataifa na kwamba nchi hizo mbili zinaweza kushirikiana na katika nyanja za kugundua na kuchimba mafuta mashariki mwa Bahari ya Mediterranean.

Hati ya maelewano ya ushirikiano wa baharini iliyosainiwa na Uturuki na serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imekabiliwa na upinzani mkali wa nchi za Misri na Ugiriki.

Waziri Mkuu wa Libya Fayez al-Sarraj,na Erdogan

Spika wa Bunge la Misri Ali Abdel Aal amesema kuwa nchi yake haitaruhusu dola lolote la kigeni kucheza katika mipaka yake na Libya na kwamba Cairo inapinga hati ya maelewano iliyotiwa saini na nchi za Uturuki na Libya kuhusiana na ushirikiano wa baharini.

Vilevile serikali ya Ugiriki imemfukuza balozi wa Libya mjini Athens, kufuatia kutiwa saini hati hiyo ya maelewano. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ugiriki Nikos Dendias amesema kuwa, kutiwa saini hati ya maelewano ya ushirikiano wa baharini kati ya serikali za Ankara na Tripoli ni ukiukaji wa wazi wa sheria na mikataba ya kimataifa na kufuatia hali hiyo serikali ya Athens imempa muda wa saa 72 balozi wa Libya nchini humo awe ameondoka katika ardhi ya Ugiriki.   

Tags

Maoni