Dec 14, 2019 12:22 UTC
  • Maandamano Uingereza kupinga matokeo ya uchaguzi, Scotland yataka kujitenga

Maandamano makubwa yameripotiwa katika maeneo mbali mbali nchini Uingereza kupinga matokeo ya uchaguzi wa bunge ambapo chama cha Kihafhidhina (Conservative) cha Waziri Mkuu Boris Johnson kimepata ushindi.

Maandamano yameripotiwa katikati mwa jiji la London katika medani ya Trafalgar na pia nje ya makao rasmi ya waziri mkuu katika barabara ya 10 Downing.  Waandamanaji walikuwa wamebaba mabango yaliyoandikwa, "Boris Johnson si waziri mkuu wangu," "Pingeni utawala wa Wahafidhina" na "Wakimbizi Wanakaribishwa". Watu kadhaa wamekamatwa na vikosi vya usalama katika maandamano hayo. Matokeo ya uchaguzi wa Uingereza yanaonyesha kuwa, chama cha Wahafidhina kimepata viti 365 kati ya viti 650 vya Bunge kikifuatiwa na chama cha Leba kinachoongozwa na Jeremy Corbyn kilichopata viti 203.

Katika mji mkuu wa Scotland, Glasgow, eneo ambalo chama cha Wahafidhina kimeshindwa vibaya, wananchi wameandamana kupinga ushindi wa Johnson. 

Maandamano ya Waskochi wanaotaka kujitenga na Uingereza

Wakati huo huo kiongozi wa Chama cha Kitaifa cha Scotland (SNP) Nicola Sturgeon, ambaye chama chake kimepata viti 48 kati ya 59, amesema wiki ijayo ataanzisha mchakato wa kutaka eneo hilo lijitenge na Uingereza.

Sturgeon amesema atatangaza mpango wa kuhamisha madaraka kutoka kwa serikali ya Johnson ili watu wa Scotland wawe na haki ya kidemokrasia ya kushiriki katika kura ya maoni ya kujitenga na Uingereza. Hata hivyo Johnson amempigia simu Sturgeon na kusema anapinga vikali kura ya maoni ya kujitenga na Uingereza.

Johnson anaongoza mkakati wa Uingereza kujitenga na Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit lakini chama cha SNP kinasema Scotland inataka kubakia katika umoja huo jambo ambalo limeibua msuguano baina ya pande mbili.

 

Tags

Maoni