Jan 16, 2020 02:31 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS), Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo ndio pekee wanaosherehekea na kufurahia kuuliwa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Dakta Zarif alisema hayo jana Jumatano katika Kongamano la Usalama katika mji mkuu wa India, New Delhi na kueleza bayana kuwa, "Watu wa matabaka yote walimiminika katika barabara za miji na nchi mbalimbali duniani kuomboleza mauaji ya kikatili ya Jenerali Soleimani ghairi ya watawala wa Washington na kundi la kitakfiri la Daesh."

Amesisitiza kuwa, "Serikali ya Marekani haikumpenda Jenerali Soleimani licha ya kwamba alikuwa na nafasi kubwa katika mapambano dhidi ya Daesh. Iwapo huniamini, tizama namna (wawatala wa Wamarekani) wanavyosherehekea (mauaji hayo), sio raia wa Marekani."

Waziri Zarif amebainisha kuwa, miji 430 ya India ilihuzunishwa na kusononeshwa na mauaji ya Soleimani na hata kufanya matembezi, vikao na marasimu ya kumuomboleza, lakini Trump, Pompeo na Daesh walifurahishwa na ukatili wao huo.

Dakta Zarif na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi

Ameashiria kuhusu kukinzana kwa matamshi ya watawala wa Washington na kusema kuwa, "Marekani ilidai kuwa Jenerali Soleimani alipanga njama za kuanzisha vita dhidi ya Marekani kwa kushambulia balozi nne za Washington nchini Iraq, lakini hivi sasa imefichuka kuwa, Trump alipanga mauaji hayo miezi saba iliyopita; hata kabla ya kuanza maandamano ya Wairaqi walioghadhabishwa na kitendo cha Washington cha kuua wanachama 25 wa harakati ya kujitolewa wananchi ya Hashdu Shaabi."

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekumbusha kuwa, Marekani haijawahi kuleta amani na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi, na ushahidi wa wazi ni hali ya ukosefu wa usalama katika nchi za Iraq na Afghanistan ambazo Washington ilizivamia kwa kisingizio cha kurejesha usalama.

Tags

Maoni