Jan 17, 2020 02:48 UTC
  • Kufichuka siri ya Trump alivyoishinikiza Troika ya Ulaya itekeleze 'Utaratibu wa Kifyatuo' katika JCPOA

Licha ya madai zinayotoa nchi za Ulaya kuhusu ulazima wa kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Troika ya nchi hizo inayoundwa na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, siku ya Jumanne ya tarehe 14 Januari iliamua kutekeleza utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika JCPOA, ambao kimsingi unatoa kitisho kwa Iran cha kuwekewa tena vikwazo vya nyuklia vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hivi sasa yamefichuka na kudhihirika mengine mapya kuhusu kilicho nyuma ya pazia la hatua hiyo iliyochukuliwa na nchi hizo tatu za Ulaya. Toleo la siku ya Jumatano ya tarehe 15 Januari la gazeti la Washington Post lilizinukuu duru za kuaminika ndani ya Umoja wa Ulaya zikiripoti kuwa, wiki iliyopita, serikali ya Trump iliwatishia kisirisiri maafisa wa nchi tatu za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kwamba Marekani itayawekea ushuru mpya wa asilimia 25 magari yanayotoka nchi hizo, vyenginevyo watekeleze utaratibu wa kusuluhisha mzozano katika JCPOA, unaojulikana kama "Utaratibu wa Kifyatuo", kwa kimombo "Trigger Mechanism". Afisa mmoja wa Ulaya ambaye hakutaja jina lake litajwe amelieleza gazeti hilo kuwa, serikali ya Marekani haikutoa kitisho hicho kupitia balozi zake, bali imefikisha taarifa za moja kwa moja kwa serikali za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza.

Viongozi wa Troika ya Ulaya: Kutoka kushoto ni Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani

Hata kama katika wiki za karibuni baadhi ya maafisa waandamizi wa nchi za Ulaya akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian, wamesikika wakitamka kuwa, wamo mbioni kuchunguza utekelezaji wa utaratibu huo, lakini kwa kutilia maanani kwamba Marekani ndiye mshirika mkuu wa kibiashara wa Umoja wa Ulaya, inaonesha vitisho vya serikali ya Trump vimechangia pia kuishinikiza Troika ya umoja huo itekeleze utaratibu huo wa kusuluhisha mzozano katika JCPOA.

Makubaliano ya nyuklia yalifikiwa rasmi Juni mwaka 2015 kati ya Iran na nchi za kundi la 5+1. Lakini baada ya Donald Trump kuingia madarakani Januari 2017, alianzisha chokochoko na visingizio dhidi ya makubaliano hayo yenye umuhimu mkubwa kwa ajili ya amani na usalama wa kimataifa. Trump alisikika mara kadhaa akidai kuwa JCPOA ni makubaliano mabaya kabisa kwa Marekani; na hatimaye mnamo tarehe 8 Mei 2018 akajitoa kwenye maafikiano hayo sambamba na kutangaza uamuzi wa kuiwekea Iran vikwazo vya upande mmoja katika awamu mbili, vikiwemo vya uuzaji mafuta. Donald Trump anataka makubaliano ya JCPOA yavunjwe na kuanzishwa mapatano mengine mapya na Iran, ambayo kwa madai yake, yatazingatia wasiwasi na matakwa yote ya Washington kuhusiana na sera na hatua zinazochukuliwa na Iran.

Licha ya Umoja wa Ulaya pamoja na Troika yake kutoa ahadi chungu nzima za kuchukua hatua zitakazopunguza taathira hasi za vikwazo vya Marekani, kama kuanzisha mfumo maalumu wa mabadilishano ya kifedha na kibiashara na Iran, ujulikanao kama INSTEX, lakini ukweli ni kwamba hadi sasa hazijafanya lolote lile la maana. Kutokana na muamala huo wa nchi za Ulaya, Iran kwa upande wake ikaamua kuchukua hatua kupitia awamu tano zilizopishana kwa muda wa siku 60 kila moja, za kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA. Katika kufanya hivyo, Jamhuri ya Kiislamu imesisitiza kuwa, kupunguza uwajibikaji huo ambako kumefanyika kulingana na vifungu vya 26 na 36 vya makubaliano ya nyuklia hakumaanishi kwamba imeyakiuka makubaliano hayo. Mnamo mwezi Mei 2019 na baada ya kutangaza awamu ya kwanza ya kupunguza kiwango cha utekelezaji wa makubaliano ya JCPOA, Iran ilieleza bayana kuwa, haitakuwa tayari tena kutekeleza peke yake makubaliano hayo ya nyuklia; na kwamba itaendelea kuyatekeleza tena kikamilifu pale tu upande wa pili, nao pia utakapotekeleza ahadi na majukumu yake.

Maafisa waandamizi wa pande husika baada ya kufikia makubaliano ya nyuklia JCPOA Juni, 2015

Suala muhimu lililodhihirika hivi sasa baada ya hatua ya kiuadui ya nchi za Ulaya ya kuamua kutekeleza utaratibu wa kuzuluhisha mzozano, kwanza ni udhaifu wa nchi hizo wa kushindwa kuikabili Marekani pamoja na hatua zao za kutapatapa zinazochukua. Lakini pili, ni utumiaji mkubwa wa 'silaha ya ukali wa wastani' unaofanywa na Marekani, ambayo ni silaha ya nguvu za kiuchumi kupitia ususiaji na uwekaji vikwazo vya kiuchumi kwa ajili ya kufikia malengo yake katika uga wa siasa za nje. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif amezikosoa nchi za Ulaya kwa kufuata siasa haribifu za Marekani kuhusiana na JCPOA na kubainisha kwamba, uchumi mkubwa zaidi wa dunia uko tayari kuzihalifu ahadi zake kwa kuridhia kuburuzwa na kufanyiwa ubabe.

Serikali ya Trump inaamini kuwa, ili kufikia malengo yake kuhusiana na nchi zingine, kutoa mashinikizo hasa ya kuweka vikwazo kwa kutumia nguvu ya 'ukali wa wastani', ni wenzo athirifu na wenye ufanisi. Hivi sasa Washington imetishia kuyatoza ushuru mpya magari yanayoingizwa nchini Marekani ili kuzilazimisha nchi za Ulaya zinazouza magari hayo zitekeleze matakwa yake kuhusiana na JCPOA. Hatua hii ni sawa na kuziadhibu kibiashara nchi za Ulaya na hasa Ujerumani ambayo uchumi wake unategemea zaidi uuzaji bidhaa nje. Ukweli ni kwamba, Trump hajali kuziwekea vikwazo na kuziadhibu kibiashara na kiuchumi hata nchi waitifaki wa Marekani wa barani Ulaya, katika kutekeleza sera yake ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kutumia nguvu na mabavu katika uga wa kimataifa ili kuifanya Washington iwe na sauti ya juu katika uga huo.../

Tags

Maoni