Jan 17, 2020 02:50 UTC
  • Mazungumzo ya Marekani na Korea Kusini kuhusu gharama za uwepo wa askari wa Kimarekani nchini humo yavunjika

Kwa mara nyingine tena mazungumzo ya viongozi wa Marekani na Korea Kusini kuhusiana na utatuzi wa tofauti zinazohusu uchangiaji wa gharama za kuendelea kuwepo askari wa Marekani na zana za kijeshi za nchi hiyo ya Magharibi katika Rasi ya Korea, yamevunjika.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini imetangaza kwamba katika duru ya sita ya mazungumzo hayo nchini Korea Kusini serikali za Seoul na Washington zimeshindwa kufikia mwafaka kuhusiana na namna ya kuchangia gharama za uwepo wa askari wa Marekani na pia kuhusu zana za kijeshi za nchi hiyo katika eneo hilo. Hivi karibuni Mark Esper, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alinukuliwa akisema kuwa, Korea Kusini ni lazima iongeze gharama za kudhamini kuendelea kuwepo askari wa Kimarekani nchini humo. Mazungumzo ya kabla ya hapo kati ya nchi mbili pia yalishindwa kufikia natija kutokana na mienendo mibaya ya Washington ya kuiwekea mashinikizo serikali ya Seoul.

Kuendelea kuwepo askari wa kigeni wa Marekani nchini Korea Kusini, kitandawili kisichoteguliwa

Marekani inaitaka nchi hiyo ya Asia kulipa karibu dola bilioni tano kwa ajili ya kuchangia gharama za kuendelea kuwepo askari hao wa kigeni nchini Korea Kusini mwaka huu 2020. Karibu askari elfu 28,500 wa Marekani wamekuwepo Korea Kusini tangu mwaka 1991 hadi sasa ambapo mwaka jana serikali ya Seoul iliipatia Washington kiasi cha dola milioni 870 kama zawadi kutokana na ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi mbili. Uchunguzi wa maoni unaonyesha kwamba akthari ya raia wa Korea Kusini wanapinga uwepo kijeshi wa askari wa Marekani katika nchi yao, kama ambavyo wanapinga pia ongezeko la gharama za ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi mbili hizo.

Tags

Maoni