Jan 17, 2020 07:40 UTC
  • India yasema ina hamu ya kuimarisha uhusiano wake na Iran

Waziri Mkuu wa India amesema nchi yake ina hamu kubwa ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nyuga tofauti.

Narendra Modi alisema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo yake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif mjini New Delhi na kuongeza kuwa, "India imejitolea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kidugu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hususan katika uga wa biashara. Tunashukuru na kupongeza pia hatua zilizopigwa katika Bandari ya Chabahar ambayo itakuwa na mchango mkubwa katika kuimarika uhusiano wa kibiashara wa pande mbili."

Mwaka 2018, maafisa wa Iran, India na Afghanistan walisaini hati ya ushirikiano kwa lengo la kupanua na kustawisha Bandari ya Chabahar iliyoko kusini mashariki mwa Iran. Kadhalika Waziri Mkuu wa India amesema nchi yake inapenda kuona amani na uthabiti vinatawala katika eneo la Asia Magharibi kwa maslahi ya pande zote. 

Kwa upande wake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif amesema Tehran inajivunia kuwa na uhusiano uliokita mizizi na New Delhi na kueleza bayana kuwa, fursa ya kupanuliwa uhusiano huo ipo.

 Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif

Aidha ameashiria mpango wa Benki ya Pasargad ya Iran wa kufungua tawi lake nchini India kwa ajili ya kuwepesisha mabadilishano ya kifedha kati ya nchi mbili hizi. 

Dakta Zarif ameongeza kuwa, "Kuna njia nyingi za kupatia ufumbuzi tatizo hilo la miamala ya kifedha, kama vile kutumia mbinu ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa au kutumia sarafu za nchi husika katika miamala ya kimataifa badala ya kutegemea dola." 

Tags

Maoni