Jan 18, 2020 02:53 UTC
  • Kukosolewa njama za Marekani za kukatiwa bajeti Shirika la UNRWA

Tangu Rais Donald Trump wa Marekani ashike hatamu za uongozi na kuingia katika ikulu ya nchi hiyo White House, alichukua mkondo wa kuuunga mkono kibubusa na bila masharti yoyote utawala haramu wa Israel na siasa za kuwa dhidi ya Wapalestina.

Agosti 31 mwaka 2018, serikali ya Trump ilikata misaada yote ya kifedha kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNRWA). Serikali ya Trump ambayo kila mara imekuwa ikichukua hatua mpya za kuwashinikiza Wapalestina, hivi sasa sambamba na kupuuza matatizo ya kifedha ya shirika la UNRWA, imejikita zaidi katika njama za kuhakikisha kwamba, misaada ya kifedha ya nchi nyingine kwa asasi hiyo inayofanya shughuli zake chini ya Umoja wa Mataifa nayo inakatwa na kusimamishwa.

 Christian Saunders, Kaimu Kamishna wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la  Umoja wa Mataifa (UNRWA), Alkhamisi iliyopita ya tarehe 16 Januari aliituhumu Marekani kwamba, inafanya mazungumzo na Mabunge ya nchi za kigeni ili yasitishe misaada yao kwa shirika hilo.

Saunders amesema kuwa: Marekani inaunga mkono suala la kukatiwa misaada ya kifedha Shirika la UNRWA katika Mabunge ya Ulaya na mataifa mengine ya dunia. Shirika la (UNRWA) linafanya shughuli zake kwa kibali cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuanzia Agosti 2018 limekuwa lilikabiliwa na matatizo ya bajeti yaani baada ya Marekani ambayo ni mfadhili mkubwa kabisa kukatisha misaada yake ambapo kwa mwaka ilikuwa ikitoa kiasi cha dola milioni 360.

Licha ya kuwa, Kaimu Kamishna wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la  Umoja wa Mataifa (UNRWA), ametoa hakikisho akisema kuwa, kwa uchache msimu wa kwanza wa mwaka huu shirika hilo lina fedha za kutosha, lakini ukweli ni kuwa linakabiliwa na kibarua kigumu. Kwa mujibu wa Saundres, utawala haramu wa Israel umekuwa ukizuia shughuli za shirika hilo huko Quds Mashariki.

Lengo la hatua hiyo ya utawala wa Tel Aviv ni kushadidisha hali mbaya ya Wapalestina na kuwalazimisha wahajiri na kuyahama maeneo hayo.  Marekani na Israel zinalituhumu Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) kwamba, lina uongozi mbaya na limekuwa likichochea hisia dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais Donald Trump wa Marekani

Licha ya tuhuma mbalimbali za Marekani na Israel kuhusiana na utendaji ulio dhidi ya Israel na kwamba, UNRWA ina ufisadi wa kifedha, lakini baada ya kukamilika uchunguzi kuhusiana na kadhia hiyo, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amethibitisha kwamba, hakuna ufisadi wala matumizi yoyote mabaya ya fedha yaliyotokea katika taasisi hiyo. Disemba mwaka jana, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliongeza kwa muda wa miaka mitatu mingine kibali cha shughuli za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA). Baada ya Marekani kukata misaada yake kwa shirika hilo la UNRWA ilitoa wito wa kufungwa shughuli za shirika hilo ikidai kwamba, namna ya kuwasaidia Wapalestina inapaswa kubadilishwa.

Jason Greenblatt, mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Asia Magharibi alisema mwishoni mwa mwaka ulimalizika hivi karibuni kwamba: Umewadia wakati sasa kwa huduma zinazotolewa na UNRWA kukabidhiwa asasi za kiraia na mataifa ambayo yamewapokea wakimbizi wa Kipalestina.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) liliasisiwa tarehe 8 Disemba 1949 kwa mujibu wa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa shabaha ya kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina na kwa sasa linawasaidia takribani wakimbizi milioni 5 waliopo katika nchi za Jordan, Syria, Lebanon na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Sami Abu Zuhri, msemaji wa Harakati ya Mpambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS anasema: Hatua ya Marekani ya kukatisha misaada yake ya kifedha kwa shirika la UNRWA inalenga kuzuia haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi zao za asili.

Kukatwa misaada ya kifedha ya Washington kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) na hivi sasa kuchukuliwa hatua za kuzuia mataifa mengine kulisaidia shirika hilo, ni sehemu ya siasa za Rais Donald Trump zinazolenga kuwashinikiza Wapalestina ili wakubaliane na mpango wa “Muamala wa Karne”.

Mpango wa "Muamala wa Karne" ni mpango mpya uliopendekezwa na Marekani wenye lengo la kufutilia mbali haki za raia wa Palestina. Mpango huu umeandaliwa kwa kushirikiana na kufikiwa mapatano baadhi ya nchi za Kiarabu zikiwemo Saudi Arabia, Bahrain na Imarati. Kwa mujibu wa mpango huo wa Marekani, haki ya Wapalestina ambayo imetambuliwa na azimio nambari 194 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ifumbiwe macho.

Kukatwa misaada ya UNRWA na kisha kufanyika njama ili nchi nyingine nazo zilikatie misaada shirika hilo sambamba na kutaka kufungwa kabisa shirika hilo la kimataifa, ni mlolongo wa huduma za serikali ya Marekani kwa utawala haramu wa Israel kama ilivyochukua hatua kama kuitambua Quds kama mji mkuu wa Israel, kuitambua miinuko ya Golan ya Syria kuwa ni sehemu ya mamlaka ya Tel Aviv na kufukuzwa balozi wa Palestina mjini Washington.

Tags

Maoni