Jan 18, 2020 02:56 UTC
  • Baba wa askari wa Marekani aliye Ain Assad: Sijui kama mwanangu yuko hai au amefariki dunia

Baba wa mmoja wa askari wa Kimarekani aliye katika kambi ya kijeshi ya Ain Assad nchini Iraq ameelezea wasi wasi wake mkubwa juu ya maisha ya mwanaye baada ya kupita zaidi ya wiki moja tangu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ishambulie kwa makombora kambi hiyo ya kijeshi.

Allen, mkazi wa Chicago nchini Marekani ambaye ni baba wa mmoja wa askari wa Kimarekani aliye katika kambi hiyo ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq ameieleza kanali ya televisheni ya C-SPAN ya Marekani kwamba tangu kulipojiri shambulizi hilo la Iran, hajapata taarifa yoyote kuhusu mwanaye licha ya kuwaendea mara kwa mara viongozi wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) lakini bila mafanikio. Allen ameongeza kwamba licha ya  kwamba viongozi wa Marekani walitangaza kuwa hakuna askari yeyote aliyedhurika katika shambulizi hilo la Iran kwenye kambi hiyo ya jeshi la Marekani ya Ain Assad, lakini tangu kulipojiri shambulizi hilo mwanaye hajawahi kupokea simu. Bwana Allen ambaye ana hasira kali na huzuni ameiambia kanali hiyo ya televisheni kwa kusema: "Mungu amlaani Donald Trump."

Askari wa Marekani wakiongea na mwandishi wa habari wa CNN ambapo walimuelezea wahka wao kutokana na shambulizi la Iran

Itakumbukwa kwamba tarehe 8 ya mwezi huu Jeshi la Walinzi wa Mapindizu ya Kiislamu ya Iran IRGC lilitoa jibu kali ikiwa ni katika kujibu jinai za jeshi la Marekani baada ya kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha jeshi hilo la Iran. Katika jibu hilo IRGC ilishambulia kwa makombora kambi ya kijeshi ya Ain Assad ya Marekani katika mkoa wa Al-Anbar na kambi nyingine ya kijeshi ya nchi hiyo vamizi katika mkoa wa Erbil nchini Iraq. Baadhi ya duru za habari zimeeleza kwamba askari wengi wa Marekani waliangamizwa na kujeruhiwa katika shambulizi hilo la ulipizaji kisasi, kiasi kwamba hakukuwepo na uwezekano wa kuwatibu katika eneo hilo na hivyo wakawa wamepelekwa kwa helikopta katika hospitali ya Marekani mjini Baghdad. Hii ni katika hali ambayo televisheni ya CNN na magazeti ya Reuters la Uingereza na Bild la Ujerumani yameripoti habari ya wahka na khofu ya hali ya juu ya askari wa Kimarakeni baada ya Iran kushambulia kwa makombora kambi hiyo ya kijeshi ya Ain Assad.

Tags

Maoni