Jan 18, 2020 07:59 UTC
  • Kamisheni ya Haki yaishtaki Marekani UN kwa mauaji ya Jenerali Soleimani

Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu (IHRC) yenye makao yake mjini London Uingereza imewasilisha malalamiko ya kuuliwa shahidi na Marekani, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC).

Katika barua hiyo kwa UN, IHRC imetoa mwito wa kubebeshwa dhima Marekani kutokana na mauaji hayo ya kigaidi ya Januari 3 karibu na Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Baghdad nchini Iraq.

Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu inasisitiza kuwa, "jinai hiyo haipaswi kufumbiwa macho na jamii ya kimataifa."

Taasisi hiyo ya haki za binadamu ya London imeunga mkono mwito wa Agnes Callamard, Ripoti Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya jinai za mauaji ambaye Januari 6, alimuomba Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres aunde jopo la kuchunguza mauaji hayo ya Soleimani, kwa mujibu wa kifungu cha 99 cha Hati ya UN. 

Rais Trump aliyetoa agizo la kuuawa kigaidi Jenerali Soleimani

Tarehe 3 Januari mwaka huu, jeshi la Marekani lilimuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq tena uraiani. Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Shaabi, Abu Mahdi al Muhandis na wenzao wanane waliuliwa kigaidi na wanajeshi wa Marekani katika shambulio hilo la kikatili lililokanyaga sheria zote za kimataifa. 

Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya CNN, serikali ya Donald Trump hadi sasa inaendelea kukwepa kuwasilisha ripoti ya mauaji ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani kwa Baraza la Congress la nchi hiyo. Maafisa wa White House wamekuwa wakikinzana wakijaribu kuhalalisha mauaji hayo ya kigaidi.

Tags

Maoni