Jan 18, 2020 14:53 UTC
  • CNN: Marekani inakaribia kuondoka kimadhila katika ardhi ya Iraq

Kanali ya televisheni ya CNN imeeleza kuhusu kuongezeka mashinikizo ya kulitaka jeshi la Marekani liondoke Iraq na kubainisha kuwa: Huo ni mwisho wa kimadhila wa kazi maalumu na ya muda mrefu iliyofanywa na jeshi la Marekani; kazi ambayo imeteketeza mabilioni ya dola.

Katika ripoti maalumu iliyotoa katika matangazo yake ya leo, CNN imeashiria ahadi hewa alizotoa Donald Trump za kuhitimisha vita visivyo na kikomo katika eneo la Asia Magharibi na kueleza kwamba: "Kuondoka kwa lazima katika ardhi ya Iraq utakuwa ndio mwisho wa kimadhila wa utekelezaji kazi maalumu iliyochukua muda mrefu ya jeshi la Marekani; kazi ambayo imeteketeza mabilioni ya dola ya fedha za walipakodi wa Marekani na kutoa roho za maelfu ya askari wa Marekani."

Ripoti hiyo ya CNN imebainisha kuwa, maafisa wa bunge la Iraq ambao wana uhusiano imara na Iran wameanzisha mchakato wa kuhitimisha kuwepo kijeshi Marekani nchini Iraq na hilo ni jibu na radamali kali kwa mauaji ya kigaidi ya Jenerali Soleimani.

Wairaqi wakidhihirisha ghadhabu na chuki zao kwa serikali ya Marekani na rais wake Donald Trump

Kanali hiyo ya televisheni ya Marekani imeongeza kuwa: Kinyume na Marekani, Iran ina stratejia madhubuti na endelevu kuhusiana na Iraq; na kuuliwa Jenerali Soleimani ni kwa faida ya malengo ya muda mrefu ya Iran, ambayo ni kuondoka Marekani katika eneo.

Usiku wa manane wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 3 Januari, majeshi ya kigaidi ya Marekani yalifanya shambulio la ndege isiyo na rubani katika uwanja wa ndege wa Baghdad, Iraq na kumuua shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Naibu Mkuu wa harakati ya Al-Hashdu-Sha'abi Abu ya Iraq, Mahdi Al-Muhandis pamoja na wanamuqawama wengine wanane waliokuwa pamoja nao.

Kamanda Soleimani alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.

Kufuatia jinai hiyo ya kigaidi iliyofanywa na Marekani katika uwanja wa ndege wa Baghdad, bunge la Iraq lilipitisha mpango wa kuwatimua askari wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani uliojiingiza nchini humo kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la DAESH (ISIS).../

Tags

Maoni