Feb 15, 2020 07:50 UTC
  • Takwa rasmi la Venezuela kwa Mahkama ya Jinai ICC kwa ajili ya kuchunguzwa jinai za Marekani

Katika kipindi cha utawala wa Rais Donald Trump Marekani imefanya jitihada nyingi za kutaka kuiondoa madarakani serikali ya mrengo wa kushoto ya Venezuela inayoongozwa na Rais Nicolás Maduro na badala yake kuiingiza madarakani serikali kibaraka itakayoongozwa na Juan Guaidó.

Katika mwenendo huo Marekani imetumia nyenzo tofauti kuiwekea vikwazo nchi hiyo. Hatua hiyo ya serikali ya Trump imekabiliwa na radiamali kali kutoka kwa serikali ya Caracas. Katika uwanja huo, Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahkama ya Kimataifa ya Jinai ICC ya The Hague Uholanzi, ametaka kufanyika uchunguzi kuhusiana na jinai dhidi ya binaadamu zilizotekelezwa na watawala wa Marekani kupitia vikwazo dhidi ya Venezuela. Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesema kuhusu suala hilo kwamba, serikali ya Caracas imeikabidhi mahkama hiyo mashtaka yake dhidi ya Washington yakiwa katika kurasa 60. Faili hilo liliwasilishwa kwa Fatou Bensouda siku ya Alhamisi. Kuhusiana na suala hilo, serikali ya Venezuela imesema kuwa vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo vina maana ya 'kutoa hukumu ya kifo' dhidi ya makumi ya maelfu ya Wavenezuela. Marekani hasa baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump mwenye utata mwingi, imeiwekea vikwazo vingi Venezuela, huku kila wakati ikiendelea kuweka vikwazo vipya dhidi ya nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta katika eneo la Amerika ya Latini. Aidha serikali ya Trump na katika hatua ya uingiliaji wake imemtangaza Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani kuwa rais wa nchi hiyo. Tayari Mahkama ya Jinai ya Kimataifa ya ICC inawafuatilia watu kadhaa, ingawa katika nyaraka zilizowasilishwa na serikali ya Caracas, hakujatajwa jina la kiongozi yeyote wa Marekani.

Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahkama ya Kimataifa ya Jinai ICC ya The Hague, Uholanzi

Katika uwanja huo Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amesema: "Kuainishwa mtu inayehusika na jinai, ni jukumu la mahkama hiyo." Kwa mujibu wa Arreaza faili hilo limewasilishwa kwa mahkama ya ICC pamoja na barua nyingine ya Rais Nicolás Maduro. Waziri huyo wa Venezuela amesisitiza kuwa: "Serikali yetu imekimbilia sheria za kimataifa. Tunaamini kwamba matokeo ya hatua za upande mmoja za Marekani, zimesababisha jinai dhidi ya binaadamu na dhidi ya raia wa Venezuela." Hata hivyo waraka huo ambao serikali ya Venezuela imeusasilisha katika Mahkama ya Kimataifa ya Jinai ICC dhidi ya Washington kwa anwani ya 'adui' wake hautapelekea kuanzishwa uchunguzi moja kwa moja, na wala mahkama hiyo huwa haifuatilii masuala yanayozihusu nchi mbili. Pamoja na hayo, kusajiliwa waraka huo na serikali ya Caracas katika mahkama hiyo, kunathibitisha jinai za muda mrefu zilizo dhidi ya binaadamu za Marekani kupitia vikwazo vya aina mbalimbali kuwalenga watu wa Venezuela kwa lengo la kuwalazimisha kumuwekea mashinikizo Rais Nicolás Maduro ili akubali ubeberu wa Washington kwa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta. Katika uwanja huo, tarehe 20 Januari mwaka huu na baada ya kukutana na Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani kando ya mkutano wa kieneo mjini Bogota, mji mkuu wa Colombia, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alisema: "Marekani itachukua hatua zaidi kwa ajili ya kumuunga mkono Juan Guaidó." Ni miezi kadhaa sasa ambapo serikali ya Trump inatekeleza hatua zake kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya mrengo wa kushoto ya Venezuela na pia kumuondoa madarakani Rais Maduro.

Juan Guaidó, kiongozi wa wapinzani ambaye ni kibaraka wa Marekani

Marekani inakusudia kumuondoa madarakani Rais Maduro kwa kumuunga mkono wazi wazi Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani na kumtangaza kuwa rais wa Venezuela, kutumia viabaya nyenzo za kiuchumi na kueneza vita vya kisaikolojia propaganda dhidi yake. Hatua za hivi karibuni za serikali ya Trump katika uga huo ni pamoja na kumwalika Juan Guaidó kuhudhuria hotuba ya kila mwaka ya rais huyo wa Marekani katika Bunge la Kongresi na kisha kukutana naye ndani ya Ikulu ya White House na kadhalika kutangaza vikwazo vipya dhidi ya Venezuela sambamba na kuliwekea vikwazo shirika la ndege la nchi hiyo. Katika miaka miwili ya hivi karibuni, Venezuela imeipitia hali mbaya ya kisiasa na kiuchumi kutokana na ongezeko la mashinikizo ya kila upande ya Marekani. Aidha kwa mtazamo wa sheria za kimataifa na pia za Umoja wa Mataifa, serikali ya Trump inatambulika kuwa iliyo kinyume cha sheria kutokana na hatua zake za kuingilia wazi wazi masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini. Pamoja na hayo Washington na katika uga wa siasa zake za upande mmoja na utumiaji mabavu, ipo tayari kwa thamani yoyote ile, kukanyaga hata sheria na mikataba ya kimataifa kwa ajili tu ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Venezuela. Suala hilo ndilo limeifanya serikali ya Caracas kuitaka Mahkama ya Jinai ya Kimataifa ya ICC kuchunguza jinai za Washington dhidi ya Venezuela.

Tags

Maoni