Feb 15, 2020 08:04 UTC
  • Congress ya Marekani: Madhara waliyopata wanajeshi wetu katika shambulizi la Iran Ain al Assad ni makubwa, huenda yakabakia milele

Chombo cha habari cha Baraza la Congress la Marekani kimeonya kwamba matatizo ya ubongo waliyopata wanajeshi wa nchi hiyo katika shambulio la kulipiza kisasi lililofanywa na Iran kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ain al Assad nchini Iraq ni makubwa na kuna hatari madhara hayo yakabakia kwa wananajeshi wa Marekani katika kipindi chote cha uhai wao.

Mtandao wa habari wa The Hill wenye mfungamano na Baraza la Congress la Marekani umeandika kuwa, ripoti mbalimbali za Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon zinaonesha kwamba hadi hivi sasa wanajeshi 109 wa nchi hiyo wamepata matatizo ya ubongo kutokana na shambulio la makombora la Iran katika kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ain al Assad nchini Iraq. Taarifa hiyo imeacha mlango wazi wa uwezekano wa kuongezeka idadi ya wanajeshi hao wa Marekani waliojeruhiwa katika shambulizi hilo.

Athari za shambulio la makombora ya Iran katika kambi ya Marekani ya Ain al Assad nchini Iraq ni kubwa sana

 

Mwandishi wa makala hiyo ameandika kwamba, kwa kawaida matatizo ya ubongo ni ya muda mfupi lakini pia yanaweza kuwa ya muda mrefu ambayo ni maarufu kwa jina la kitaalamu la matatizo ya ubongo ya PCS ambayo hubakia nayo muathiriwa katika kipindi chote cha uhai wake.

Tarehe 8 Januari mwaka huu, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH lilishambulia kwa makombora kambi ya kubwa zaidi ya kijeshi Marekani nchini Iraq ya Ain al Assad ikiwa ni kujibu jinai iliyofanywa na Marekani ya kumuua kigaidi, shahid Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH. 

Iran iliitwanga kwa makombora 13 mazito kambi hiyo ya wanajeshi wa Marekani iliyoko kwenye mkoa wa al Anbar wa magharibi mwa Iraq.

Tags

Maoni