Feb 16, 2020 08:13 UTC
  • Mahakama ya Rufaa ya Uingereza 'yaharamisha' ndoa za Kiislamu

Mahakama ya Rufaa ya Uingereza imebatilisha uamuzi wa miaka miwili iliyopita wa kutambua ndoa iliyofanyika kwa mujibu wa sheria za Kiislamu (Nikah).

Mahakama ya Rufaa ya Uingereza imebatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu ya nchi hiyo wa mwaka 2018, uliotambua kwamba wanandoa waliooana kwa misingi ya sheria za Kiislamu walifuata sheria ya ndoa ya nchi hiyo.

Mwanasheria Mkuu wa Uingereza ndiye aliyekata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa Agosti 2018 wa Mahakama Kuu. Kesi hiyo ilihusu kutalakiana kwa Nasereen Akhter na Mohammed Shabaz Khan ambao wana watoto wanne.

Uamuzi huu mpya wa Mahakama ya Rufaa unamaanisha kwamba, ndoa hiyo ilifanyika kinyume cha sheria na hivyo basi ni haramu.

Uamuzi wa Mahakama Kuu wa 2018 ulichukuliwa baada ya Nasreen Akhter kutalikiana na mume wake, Mohammad Shabaz Khan, ambaye alijaribu kuzuia talaka hiyo kwa kudai kuwa hawakuwa wameona kwa mujibu wa sheria za Uingereza na kwamba ndoa yao ilifanyika  'kwa mujibu wa sheria za Kiislamu tu.'

Mahakama Kuu ya Uingereza

Jaji David Williams wa Mahakama Kuu ya Uingereza wakati huo alisema wawili hao wamekuwa wakiishi kama mume na mke na hivyo ndoa yao ni halali kwa mujibu wa sheria za nchi.

Wadadisi wa mambo wanasema uamuzi huu wa Mahakama ya Rufaa ni moja ya hatua za chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu nchini Uingereza, nchi ya Ulaya yenye Waislamu karibu milioni tatu.

Tags

Maoni