Feb 17, 2020 02:41 UTC
  • Baraza la Mamufti Russia: Waislamu waunde nguvu ya kukabiliana na mpango wa Muamala wa Karne

Naibu Mkuu wa Baraza la Mamufti la Russia amesema kuwa Waislamu wanapasa kuwaunga mkono Wapalestina dhidi ya mpango wa Kimarekani wa Muamala wa Karne.

Muhyi al Dinov aliyasema hayo jana Jumapili ambapo akibainisha kwamba mpango wa Muamala wa Karne unadhamini kikamilifu maslahi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, amesema kuwa katika mazingira haya magumu nchi za Kiislamu ni lazima ziliunge mkono taifa la Palestina. Naibu Mkuu wa Baraza la Mamufti la Russia ameongeza kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani aliwasilisha mpango huo wa Muamala wa Karne kwa lengo la kuimarisha kampeni na nafasi yake katika uchaguzi ujao wa rais nchini Marekani. 

Baraza la Mamufti la Russia

Muhyi al Dinov amesema, maslahi ya taifa la Palestina hayatakiwi kufanywa muhanga wa kampeni za nchi nyingine na kwamba Waislamu kote duniani wana jukumu zito la kuwaunga mkono Wapalestina. Kwa mujibu wa Naibu Mkuu wa Baraza la Mamufti la Russia, nchi zote za Kiarabu na Kiislamu zinapasa kuzingatia suala hilo na kuhitimisha ukiukaji dhidi ya haki za taifa la Palestina. Akibainisha kuwa taifa la Palestina ni lazima liasisiwe haraka iwezekanavyo, amebainisha kwamba, Wapalestina wataweza tu kuishi kwa amani katika nchi huru na kwa msingi huo jamii ya kimataifa inapasa kusaidia kufanikisha jambo hilo.

Tags

Maoni