Feb 17, 2020 02:43 UTC
  • Wakazi wa Hong Kong waandamana kupinga vituo vya kuwaweka karantini washukiwa wa Corona

Wakazi wa mji wa Hong Kong wamefanya maandamano kwa siku mbili mtawalia wakipinga mpango wa viongozi wa mji huo wa kuyabadilisha majengo ya makazi kuwa vituo vya kuweka karantini watu wanaodhaniwa kuathirika na virusi vya Corona.

Katika maandamano ya Jumapili ya jana waandamanaji sambamba na kupinga uamuzi wa viongozi wa mji huo wa kutenga majengo kadhaa ya makazi kati ya majengo mapya yaliyojengwa kwa ruzuku ya serikali, wameukataa mpango huo wa kuwaweka karantini wadhaniwa wa virusi hivyo vya Corona katika nyumba hizo. Baadhi ya waandamanaji wamepiga nara zinazosema kuwa kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakisubiri kukabidhiwa nyumba za kuishi na hivi sasa viongozi wa Hong Kong wamezikabidhi nyumba hizo kwa wadhaniwa wa virusi vya ugonjwa huo.

Juhudi za kukabiliana na virusi vya Corona

Inafaa kuashiria kuwa bei ya nyumba mjini hapo iko juu sana ikilinganishwa na ya miji mingine ya dunia. Katika uwanja huo kumiliki nyumba mjini Hong Kong ni jambo gumu sana. Hadi sasa jumla ya kesi 57 za virusi vya Corona zimethibitishwa mjini hapo na tayari mtu mmoja amekwishafariki dunia. Baadhi ya wakazi wa mji wa Hong Kong wameitaka serikali ya mji huo kufunga mipaka yake na China kwa lengo la kuzuia kuenea mjini humo virusi vya Corona. Hata hivyo kiongozi wa eneo hilo Carrie Lam amepinga takwa hilo.

Maoni