Feb 18, 2020 12:25 UTC
  • Hatua za Donald Trump na kuongezeka umasikini nchini Marekani

Licha ya ahadi chungu nzima alizotoa Rais Donald Trump wa Marekani za kupunguza kiwango cha umasikini nchini humo, lakini idadi ya watu wanaotaabika kwa ufakiri na umasikini imeongezeka katika miaka ya hivi karibuni.

Takwimu zinaonyesaha kuwa, watoto wa Kimarekani wenye asili ya Afrika ndio waathiriwa wakuu wa umasikini nchini Marekani. Ilhan Omar, Mbunge Mwislamu wa chama upinzani cha Democrats katika Kongresi la Marekani Jumapili ya juzi aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter akikosoa vikali mazingira mabaya wanayokabiliwa nayo watoto nchini Marekani ambapo alitangaza kuwa, watoto milioni 11 wa nchi hiyo wanakabiliwa na baa la njaa. Bi Ilhan Omar alisema kuwa, akthari ya wanachuo wa Kimarekani wanalala na njaa kutokana na kutokuwa na fedha za kukimu mahitaji ya chakula.

Ilhan Omar, Mbunge Mwislamu wa chama upinzani cha Democrats katika Kongresi la Marekani 

Moja ya matatizo makubwa kwa sasa nchini Marekani ni kuongezeka umasikini na kupanuka ufa baina ya masikini na matajiri. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika miaka ya hivi karibuni tofauti za kimatabaka nchini Marekani zimeongezeka kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa, jambo ambalo limesababisha kushadidi pia ukosefu wa usawa wa kijamii na umaskini kwa ujumla.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, takribani asilimia 88 ya utajiri wa Marekani inashikiliwa na asilimia ndogo ya watu wenye kipato cha juu. Hii ni katika hali ambayo, zaidi ya Wamarekani milioni 39 wanahitajia msaada wa chakula wa serikali. Mstari wa umasikini ulioainishwa kwa familia moja ya Kimarekani ya watu wanne inayoundwa na watu wazima wawili na watoto wadogo wawili ni wa kipato cha dola 25,750 kwa mwaka.

Sera mbovu za serikali ya Trump zikiwemo za kupuunguza huduma kama za bima ya tiba kwa tabaka masikini na katika upande mwingine marekebisho ya ulipaji kodi yaliyofanywa na serikali ya Trump yamekuwa ni kwa maslahi ya tabaka lenye kipato cha juu. Aidha hatua hiyo imeandaa mazingira ya kifedha na utajiri mkubwa kwa mashirika makubwa na matajiri na hivyo kusaidia kuongezeka tofauti za kimatabaka.

Umasikini umepelekea kuongezeka ombaomba nchini Marekani

Ukweli wa mambo ni kuwa, sera na siasa hizi za Trump zinawafanya matajiri wazidi kuwa matajiri zaidi na maskini wazidi kuzama katika umasikini. Nara na utendaji wa kibaguzi wa Trump na kupunguza serikali yake huduuma za kijamii kama bima nazo zinaelezwa na weledi wa mambo kuwa zimezidi kushadidisha hali hii ya umasikini nchini Marekani.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Monmouth unaonyesha kuwa, asilimia 53 ya wananchi wa Marekani wanasisitiza kuwa, familia zenye kipato kidogo na masikini nchini humo hazijanufaika kwa vyovyote na sera za serikali ya Trump.

Kwa muktadha huo, akthari ya Wamarekani wamekata tamaa kabisa na utendaji wa sasa na wa baadaye wa serikali ya Trump katika suala zima la uchumi na hivyo wanazieleza siasa za Trump kwamba, ndizo zilizopelekea kuongezeka umasikini nchini humo na hivyo kuyafanya maisha yao kuwa magumu siku baada ya siku.

Andre Perry, mtafiti wa Chuo cha Brookings ameandika kuhusiana na suala hilo kwamba: Umasikini uliongezeka nchini Marekani katika sekta mbalimbali baina ya mwaka 2016 na 2018, kiasi kwamba, Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao ni vibarua na asilimia 63 ya vibarua wenye asili ya Amerika ya Latini wanajishughulisha na kazi zenye kipato cha chini tena katika mazingira mabaya.

Rais Donald Trump wa Marekani

Hali hiyo imelifanya suala la umasikini na tofauti za kimatabaka kuwa mada kuu ya kisiasa na mjadala muhimu wa wagombea wa Demokrats na Republican katika uchaguzi ujao wa rais nchini Marekani. Wademokrats wanataka serikali iongeze usaidizi na uungaji mkono wake kwa matabaka dhaifu katika jamii ya nchi hiyo na kuongeza kodi kwa tabaka tajiri na lenye kipato kikubwa.

Kwa hakika umasikini umeendelea kuwa tatizo kubwa nchini Marekani na kuwa na taathira hasi hususan kwa maisha ya akthari ya watoto, wanawake, Wamarekani weusi na wahajiri. Jambo hilo limeendelea kuwa sababu ya kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu katika kijamii na ukosefu wa usalama kwa Wamarekani wengi.

Hii ni katika hali ambayo, Rais Donald Trump angali anapiga ngoma ya kukua uchumi na kutengeneza taswira ya uchumi imara na wenye nguvu wa nchi hiyo. Hapana shaka kuwa, katika miezi ijayo ya kukaribia uchaguzi, kutadhihirika zaidi tatizo hili la kijamii nchini Marekani.

Tags

Maoni