Feb 19, 2020 02:51 UTC
  • China yasisitiza kuwa serikali ya Marekani ni ya kijasusi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesisitiza serikali ya Marekani imesimama katika msingi wa ujasusi wa kimtandao duniani.

Geng Shuang amesema kuwa, Marekani inapasa kujitokeza wazi  na kuibainishia jamii ya kimataifa kuhusiana na suala hilo na itoe maelezo ni kwa nini inazijasusi nchi nyingine za dunia. Aidha Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China sambamba na kuashiria kwamba kila siku Marekani huwa inadukua taarifa zinazokaribia bilioni tano za simu za mkononi na kukusanya habari zake, amebainisha kuwa kwa mwaka serikali hiyo huwa inapenyeza ujasusi ndani ya zaidi Computer milioni tatu za mashirika ya China.

Geng Shuang, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China

Matamshi ya Geng Shuang yamejiri kufuatia kutolewa taarifa zinazoashiria utumiaji wa Shirika la Kijasusi la  Marekani CIA wa taarifa za Shirika la Crypto AG la Uswisi kwa ajili ya kuzijasusi nchi nyingine za dunia. Shirika la Crypto AG linajishughulisha na kuziuzia nchi mbalimbali za dunia vifaa na mashine za kisasa ambapo Shirika la Kijasusi la  Marekani CIA huwa linaweza kudukua na kusoma namba za vifaa hivyo katika nchi 120 za dunia.

Tags

Maoni