Feb 20, 2020 07:18 UTC
  • Russia yaitisha kikao cha dharura cha UN kujadili hatua ya Marekani ya kumnyima viza mjumbe wake

Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kufanyika kikao cha dharura cha umoja huo kwa ajili ya kujadili tabia ya Marekani ya kuwanyima viza ya kuingia nchini humo wawakilishi na wajumbe wa nchi mbalimbali kwa ajili ya kushiriki katika mikutano na vikao vya mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Konstantin Vorontsov amesema kikao cha Umoja wa Mataifa kinapaswa kufanyika kikihudhuriwa na katibu Mkuu, Antonio Guterres ili kujadili hatua ya Marekani ya kuwanyima viza mkuu wa ujumbe wa Russia katika kikao cha Kamati ya Kuzuia Silaha mjini New York. 

Kamisheni ya Kuzuia Silaha ya Umoja wa Mataifa Jumanne iliyopita ilichukua uamuzi wa kuakhirisha kikao chake kwa muda wa siku 10 hadi pale kadhia hiyo itakapowekwa wazi. 

Mwezi Januari mwaka huu pia Marekani ilikataa kumpatia viza ya kuingia nchini humo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York. 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Hatua hiyo ya Washington inakiuka 'Makubaliano ya Makao Mkuu ya Umoja wa Mataifa ya 1947' ambayo yanaishurutisha Marekani kuwaruhusu kuingia nchini humo wanadiplomasia wa nchi za kigeni wanaokwenda kushiriki mikutano ya Umoja wa Mataifa.

Serikali ya Donald Trump pia imewawekea vizuizi vingi vya kutembea ndani ya mji wa New York wanadiplomasia wa baadhi ya nchi na familia zao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amekuwa akiitaka Marekani iheshimu sheria za kimataifa na makubaliano yanayohusiana na makao makuu ya Umoja wa Mataifa.   

Tags

Maoni