Feb 20, 2020 12:12 UTC
  • Watu tisa wapigwa risasi na kuuawa katika hujuma ya kigaidi Ujerumani

Watu tisa wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika hujuma ya kigaidi mjini Hanau magharibi mwa Ujerumani iliyotokea Jumatano usiku.

Polisi imethibitisha watu tisa wamepoteza maisha na wengine watano wamejeruhiwa. Polisi katika mji huo  wamesema mshukiwa wa shambulio, aliyekuwa na umri wa miaka 43,  amekutwa amefariki nyumbani kwake. Aidha pembeni mwa mwili wa mshukiwa huyo polisi wamepata mwili wa mama yake aliyekuwa na umri wa miaka 72. Wawili hao wamefariki kutokana na majeraha ya risasi. Waziri wa mambo ya ndani katika eneo hilo Peter Beuth amesema jumla ya waliofariki katika tukio hilo ni watu 11, akiwemo mshukiwa,  huku mtu mwingine akijeruhiwa vibaya.

Shambulio hilo lilitokea usiku wa jana katika baa mbili za shisha katika maeneo tofauti.

Kwa mujibu wa taarifa, washambuliaji walifyatua risasi katika baa ya kwanza katikakati mwa mji wa Hanau na kuwaua watu watatu, na kisha baadaye walielekea mtaa jirani wa Kessel-stadt na kufyatua risasi tena katika baa nyingine ambapo watu watano waliuawa.

Hanau ni mji ulio katika jimbo la Hesse kilometa chache kutoka Frankfurt. Polisi Ujerumani wameanzisha uchunguzi huku kukiwa na tetesi kuwa gaidi aliyetekeleza hujuma hiyo ni mzungu mwenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia. Wafuasi wa mrengo wa kulia wanapinga kuweko watu wenye asili ya kigeni nchini Ujerumani na maeneo mengine Ulaya.

Tags

Maoni