Feb 20, 2020 12:25 UTC
  • China mbioni kutibu wagonjwa wa COVID-19 (Corona),  vitanda vya hospitali vyaongezwa

China imetangaza kuwa inafanya juhudi zote kuwatibu wagonjwa wa homa ya COVID-19 inayosababishwa na virusi vya Corona katika mji wa Wuhan ambao ndio kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo.

Serikali ya China inasema idadi ya vitanda vya hospitali kwa ajili ya wagonjwa wa COVID-19 imeongezeka na kuzidi elfu 40, huku idadi ya wafanyakazi wa afya waliojitolea kutoka nje ya mkoa, ikizidi elfu 30.

Naibu waziri mkuu wa China Bi. Sun Chunlan ambaye ni kiongozi wa timu ya serikali kuu ya kuelekeza kazi ya udhibiti wa mlipuko wa virusi vya Corona, aliwatembelea wafanyakazi wa afya walioko katika mstari wa mbele mjini Wuhan ambapo amesisitiza kuhusu wagonjwa kutibiwa kwa juhudi zote.

Bi. Sun amesema ni muhimu kujumuisha uzoefu kwa wakati na kuweka itifaki maalumu za matibabu.

Afisa huyo pia ametoa wito wa juhudi za pamoja kufanywa kuwatibu wagonjwa mahututi ili kupunguza kiwango cha vifo vinavyotokana na virusi vya Corona.

Hadi kufikia 19 Februari, watu 2,118 walikuwa wamepoteza maisha China kutokana na virusi vya Corona na wengine 74,576 tayari wameshaambukizwa ugonjwa huo tokea uripotiwe mara  ya kwanza mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2019.

Tags

Maoni