Feb 22, 2020 03:41 UTC
  • Wajerumani waandamana kupinga mashambulizi ya kibaguzi ya Hanau, ulinzi wazidishwa kwenye misikiti

Maelfu ya Wajerumani wamefanya maandamano katika miji kadhaa ya nchi hiyo wakilaani mashambulizi ya kibaguzi yaliyotokea katika eneo la Hanau lililoko karibu ya mji wa Frankfurt.

Maandamano hayo ya kupinga ubaguzi yamefanyika katika zaidi ya miji 50 ya Ujerumani ambako waandamanaji wamelaani vikali mashambulizi yaliyofanywa na raia mmoja wa nchi hiyo aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada na ya kibaguzi katika mji wa Hanau. 

Wakati huo huo serikali ya Ujerumani imezidisha ulinzi katika maeneo ya misikiti ya Waislamu nchini humo. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Horst Seehofer, amesema kuwa idadi ya polisi itazidishwa katika misikiti na maeneo mengine nyeti yanayoweza kushambuliwa. 

Polisi ya Ujerumani imezidisha ulinzi kwenye misikiti

Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier ambaye Alkhamisi iliyopita alijiunga na maelfu ya watu waliokusanyika kutoa mkono wa pole kwa familia za watu waliouawa katika mashambulizi ya kibaguzi la Hanau amesema kuwa shambulio hilo lilikuwa mauaji ya kinyama na kuongeza kuwa: Mahudhurio ya maelfu ya watu au mamia ya maelfu ya Wajerumani katika maandamano ya kuonyesha msikamano na kutoa pole kwa wafiwa yanaipa nguvu serikali ya Ujerumani katika mapambano dhidi ya chuki. 

Watu 9 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika hujuma ya kigaidi mjini Hanau huko magharibi mwa Ujerumani iliyotokea Jumatano usiku. Ripoti zinasema hali za majeruhi wa shambulizi hilo ni mbaya sana. 

Polisi ya Ujerumani imetangaza kuwa mtu aliyefanya mashambulizi hayo dhidi ya maeneo yanayotumiwa zaidi na Waarabu ni raia wa nchi hiyo, Tobais Rathjen, 43, ambaye aliandika barua akieleza fikra zake za kibaguzi na kinazi na baadaye akajiua mwenyewe. 

Tags

Maoni