Feb 26, 2020 04:32 UTC
  • Guterres ataka kuzidishwa jitihada za kushughulikia tatizo la wakimbizi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuzidishwa jitihada za kukabiliana na tatiizo la uukimbizi kote duniani.

Antonio Guterres ambaye alikuwa akizungumza jana katika Jukwaa Kuu la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lililohudhuriwa na wanafikra, wataalamu, wanasiasa wa zamani na wachambuzi wa masuala ya kisiasa huko Geneva, amesema kuwa, ni jambo lisilokubalika kuona mamilioni ya watu wakifukuzwa katika nyumba na makazi yao kwa njia za kinyama bila ya tatizo hilo kupatiwa ufumbuzi. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, tatizo la wakimbizi halipaswi kuwa mgogoro wa kudumu na ametaka kubuniwe fikra mpya zitakazowasaidia wakimbizi na kupata ufumbuzi wa haraka wa tatizo hilo.

UN: Watu milioni 70 wamelazimishwa kukimbia makazi yao

Jukwaa Kuu la Wakimbizi lilianzishwa Novemba mwaka 2019 kwa amri ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kwa shabaha ya kuchunguza changamoto za kimataifa na kukutanisha pamoja nguvu za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa wakimbizi. 

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa watu milioni 70 wamelazimishwa kukimbia makazi na nyumba zao katika maeneo mbalimbali ya dunia na kwamba, idadi hiyo ni mara dufu ikilinganishwa na ile ya miaka 20 iliyopita.

Zaidi ya wakimbizi milioni 25 ni wale waliovuka mipaka na hawawezi kurejea katika nchi zao. 

Tags