Feb 27, 2020 02:24 UTC
  • Ghasia za umwagaji damu baina ya wapingaji na waungaji mkono wa sheria mpya ya uraia nchini India

Kwa akali watu 23 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 150 wamejeruhiwa katika mji mkuu wa India New Delhi, kufuatia ghasia zilizoibuka kati ya wapingaji na waungaji mkono wa sheria tata ya kuwapa uraia wa nchi hiyo watu wasio Waislamu.

Ghasia na mauaji hayo yametokea wakati Rais Donald Trump wa Marekani alipokuwa ziarani nchini humo. Ghasia hizo ziliibuka baada ya maelfu ya wapingaji kufanya maandamano na kuvamiwa na waungaji mkono wa sheria hiyo yenye utata ambapo licha ya polisi kutumia mabomu ya kutoa machozi, hawakuweza kuzima vurugu hizo. 

Sheria mpya ya uraia nchini India ambayo inaandaa mazingira ya kupatiwa uraia wahajiri wasiokuwa Waislamu, inalalamikiwa na jamii ya Waislamu nchini humo, asasi za kiraia na hata baadhi ya wanachama waandamizi wa chama tawala nchini humo cha Bharatiya Janata (JBP) ambao wanasema kuwa, sheria hiyo ni ya kibaguzi. Kwa hakika kupasishwa sheria hiyo mpya nchini India ni mwendelezo wa siasa za chuki na uhasama za serikali ya New Delhi dhidi ya Waislamu.

Maandamano ya wananchi wa India ya kupinga sheria ya uraia inayowabagua Waislamu

Chama cha mrengo wa utaifa cha Bharatiya Janata (BJP) ambacho ndicho kinachotawala kwa sasa nchini India kiliwasilisha muswada wenye utata mkubwa katika Bunge la nchi hiyo msimu wa joto uliopita wa kubatilisha mamlaka ya kujitawala eneo la Kashmir. Kupasishwa muswada huo kukawa kumepigwa hatua ya kwanza ya chuki dhidi ya Uislamu.

Lengo la serikali ya India la kufuta mamlaka maalumu ya kujitawala eneo la Kashmir ambalo wakazi wake wengi ni Waislamu ni kubadilisha muundo wa kijamii wa eneo hilo kwa maslahi ya Wahindu ambapo kufutwa mamlaka ya kujitawala  eneo hilo kunaandaa mazingira ya kufikiwa lengo hilo.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, kubatilishwa mamlaka maalumu ya kujitawala Kashmir kunaandaa uwanja wa kununuliwa ardhi za eneo hilo na Wahindu na kwa muktadha huo hatua kwa hatua muuundo wa kijamiii katika eneo la Kashmir utakuwa ni kwa madhara ya Waislamu.

Nasrendra Modi, Waziri Mkuu wa India

Katika mwendelezo wa siasa hizi za chuki cha chama tawala cha Bharatiya Janata (JBP) dhidi ya Waislamu nchini India, kumepasishwa sheria mpya katika Bunge la nchi hiyo ambayo kwa mujibu wake wahajiri wasiokuwa Waislamu tu ndio watakaokuwa na haki ya kupatiwa uraia wa nchi hiyo. Uamuzi huo wa serikali ya New Delhi unakinzana wazi wazi na mikataba ya haki za binadamu ukiwemo wa kupinga ubaguzi kwa misingi ya kidini.

Kuendelea mizozo na ghasia nchini India kutokana na kutekelezwa sheria mpya ya uraia kunaonyesha kuwa, serikali ya New Delhi imeanzisha mchezo hatari ambapo anayebeba jukumu la mauaji ya baadhi ya watu baina ya wapingaji na waungaji mkono wa sheria hiyo tata ni Narendra Modi, Waziri Mkuuu wa India ambaye ana historia ndefu ya uadui na jamii ya Waislamu wa nchi hiyo.

Ghasia katika mji mkuu wa India New Delhi baina ya wapingaji na waungaji mkono wa sheria ya uraia inayowabagua Waislamu

Inaonekana kuwa, kuzuka ghasia katika mji mkuu New Delhi baina ya wapingaji na waungaji mkono wa sheria mpya ya uraia ni jambo ambalo haliwezi kufumbiwa macho na serikali ya Waziri Mkuu Modi, kwani kuendelea kwa hali hiyo kutakuwa ni changamoto kubwa kwa chama tawala katika kudhamini amani na nidhamu katika mji mkuu huo.

Tags

Maoni