Feb 27, 2020 02:25 UTC
  • Sanders: Nikichaguliwa kuwa rais nitaurejesha ubalozi wa US Tel Aviv

Seneta wa jimbo la Vermont nchini Marekani anayeongoza katika mbio za kuwakilisha chama cha Democratic katika uchaguzi ujao wa rais nchini humo amemtaja Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu kama mbaguzi asiyependa ustawi wa kisiasa na kijamii.

Bernie Sanders amesema hayo ikiwa ni siku chache baada ya kutangaza kuwa hatashiriki katika mkutano wa kila mwaka wa lobi na kundi la mashinikizo la Wayahudi wa Marekani (AIPAC) ambapo pia amefufua mjadala kuhusu hatua ya Rais Donald Trump kuuhamishia ubalozi wa US katika mji wa Quds kutoka Tel Aviv.

Sanders amemtaja Netanyahu kama mtu mwenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia, na kueleza bayana kuwa, "Ninaona fahari kuwa Myahudi, nimewahi kuishi Israel miezi michache. Lakini ninachoamini ni kuwa, kwa masikitiko na bahati mbaya hivi sasa dola la Israel linaendeshwa na Bibi Netanyahu ambaye ni mbaguzi na asiyependa mageuzi."

Kitendo cha Rais Donald Trump kuhamishia ubalozi wa nchi hiyo Quds kililaaniwa vikali kote duniani

Kadhalika ameitaka serikali ya Washington ibadili siasa na misimamo yake kuhusiana na Wapalestina huku akiahidi kuurejesha ubalozi wa Marekani mjini Tel Aviv kutoka Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.

Mwanasiasa huyo licha ya kuwa Myahudi, lakini amekuwa akikosoa vikali sera za Benjamin Netanyahu. Hivi karibuni alikosoa vikali mashambulizi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. 

Tags

Maoni