Mar 11, 2020 07:17 UTC
  • Merkel: 60% hadi 70% ya Wajerumani huenda wakakumbwa na Corona

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema yumkini asilimia 60 hadi 70 ya jamii ya nchi hiyo ya Ulaya itaambukizwa virusi vya Corona.

Merkel alisema hayo jana Jumanne mbele ya Bunge la nchi hiyo ambalo lilipokea kwa mshtuko mkubwa takwimu hizo za kuogofya za Kansela wa nchi hiyo.

Amesema ikilazimu, vikao vya Bunge la nchi hiyo ya Ulaya vitasimamishwa, sambamba na kufutwa kwa mikutano na shughuli zenye mijumuiko ya watu wengi. Hata hivyo hajaeleza serikali yake imejiandaa vipi kukabiliana na mripuko wa Corona, iwapo hali itazidi kuwa mbaya nchini humo.

China ndiyo kitovu cha virusi vya Corona na inaongoza kwa idadi ya vifo na maambukizi ya virusi hivyo

Kufikia sasa, Ujerumani ina kesi 1,400 za ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya Corona, huku watu wawili wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo nchini humo.

Italia ndiyo nchi ya Ulaya iliyoathirika zaidi na Corona, kwani kufikia sasa watu 631 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo nchini humo, huku waliombukizwa wakiwa zaidi ya elfu 10.

Tags

Maoni