Mar 15, 2020 02:28 UTC
  • Mwaka mmoja baada ya mauaji ya Waislamu New Zealand, usiri unatawala uchunguzi kuhusu mauaji hayo

Ripoti iliyotayarishwa na gazeti la Washington Post inasema kuwa, uchunguzi wa serikali ya New Zealand wa kutaka kupata majibu yanayoweka wazi jinsi mhalifu aliyefanya mauaji ya kutisha ya Waislamu 51 waliokuwa wakitekeleza ibada misikitini, alivyoweza kufanya mauaji hayo, unaendelea kwa usiri mkubwa, jambo ambalo limezusha wasiwasi wa wachambuzi wa mambo ya jamii ya Waislamu wa New Zealand.

Mauaji hayo ya halaiki ambayo yalifanyika tarehe 15 Machi mwaka jana katika mji wa Christchurch yalifuatiwa na uchuzi mkubwa na wa ngazi za juu na kusababisha mabadiliko katika kikosi cha usalama nchini New Zealand.

Mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu cha Waikato, Alexander Gillespie amesema kuwa, hujuma dhidi ya misikiti ya Waislamu nchini New Zealand zilidhihirisha kufeli kukubwa mashirika ya upelelezi na usalama. Msomi huyo amefananisha hujuma hizo na mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani.

Mhadhiri huyo amesema vyombo vya upelelezi na usalama vinakabiliwa na maswali magumu sana kuhusu hujumu hizo zilizolenga misikiti na kwa msingi huo uchunguzi wa mauaji hayo unagubikwa na usiri mkubwa.

Ripoti ya Washington Post inasema kuwa, kutokana na kuzuiwa mjadala wa wazi wa kuhusu sababu za mauaji hayo nchini New Zealand, raia wengi wamekosa majibu halisi juu ya iwapo vyombo vya usalama vilikosea kutoa tahadhari na kushindwa katika kuchunguza ripoti za siri kuhusu mtekelezaji wa mauaji ya Waislamu katika mji wa Christchurch, Brenton Tarrant.

Brenton Tarrant

Bado haijabainika wazi iwapo gaidi huyo anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji na ugaidi alisaidiwa au kushajiishwa na watu wengine au iwapo alikuwa na mahusiano na makundi ya wabaguzi wa Kizungu.

Gaidi huyo alishambulia misikiti miwili ya Al Noor na Linwood iliyopo kwenye kiunga cha mji wa Christchurch.

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern alisema wakati huo kwamba "shambulio hilo la kigaidi" lilipangwa kwa umakini.

Brenton Tarrant, gaidi mwenye chuki na Uislamu uraia wa Australia aliyefanya mauaji hayo ya kutisha, ametajwa kuwa shabiki wa hotuba za Rais Donald Trump wa Marekani.

Tags

Maoni