Mar 19, 2020 02:43 UTC
  • Machaguo mawili ya Moscow kwa makundi ya kigaidi, Idlib nchini Syria

Russia imeyapa machaguo mawili makundi ya kigaidi yananayofadhiliwa na nchi za Magharibi katika eneo la Idlib huko kaskazini mwa Syria. Mwezi Januari mwaka huu jeshi la Syria na washirika wake walianzisha operesheni ya kuusafisha mkoa huo wa Idlib, ambao ndio ngome ya mwisho ya magaidi ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Baada ya kusonga mbele jeshi hilo la Syria na washirika wake mkoani Idlib na uingiliaji kati wa jeshi wa Uturuki kwa ajili ya kuwasaidia magaidi, hatimaye kulifikiwa makubaliano ya kusitisha vita katika eneo hilo kati ya marais wa Russia na Uturuki. Katika hatua nyingine kuliundwa kituo cha uangalizi wa usitishaji vita kati ya Russia na Uturuki huko Idlib. Hata hivyo makundi ya kigaidi yameendelea kufanya mashambulizi katika eneo hilo. Suala hilo limekabiliwa jibu kali la Russia. Katika uwanja huo, Jumatatu iliyopita Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ilitoa taarifa ambayo sambamba na kukosoa kuendelea shughuli za makundi ya kigaidi likiwemo genge la Tahriru sh-Sham ndani ya mkoa wa Idlib, ilifafanua kuwa, makundi hayo ya kigaidi yametumia vibaya hali ya amani iliyopatikana na sambamba na kujizatiti upya kwa silaha, yamewashambulia ngome jeshi la serikali ya Syria. Kwa kuzingatia suala hilo serikali ya Moscow imesisitiza kwamba: "Wahusika wa ukatili na mauaji ya kigaidi wanapaswa kuchukuliwa hatua bila ya kujali uraia wao na hapa wana na machaguo mawili pekee, ama kutokomeza magaidi hao iwapo watajaribu kupambana, au wahukumiwe kwa mujibu wa sheria." 

Operesheni za jeshi la Russia za kuwafyeka magaidi wa Kiwahabi nchini Syria

Russia, kama mmoja wa pande zenye nafasi kubwa katika uga wa Syria, imekuwepo kijeshi ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu tangu mwezi Septemba 2015 na kupitia mashambulizi yake makubwa ya anga na makombora na pia ushiriki wa vikosi vya majeshi yake ya nchi kavu katika operesheni za jeshi la Syria ndani ya maeneo tofauti ya nchi hiyo ukiwemo mkoam wa Idlib, imekuwa na nafasi muhimu katika kuyaangamiza makundi ya kigaidi. Serikali ya Moscow ambayo ni mshirika wa Damascus, imeitaja Uturuki kuwa sababu ya matukio ya hivi karibuni katika mkoa wa Idlib na muungaji mkono wa makundi ya kigaidi na inaendelea kusaidia operesheni za jeshi la Syria kwa ajili ya kuyakomboa maeneo ya nchi hiyo kutoka kwenye makucha ya magaidi. Kwa mujibu wa Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia: "Jeshi la Syria linayo haki ya kupambana na magaidi katika mkoa wa Idlib." Hivi sasa ambapo magaidi wapo katika hali mbaya, mustakbali wao kwa mujibu wa mtazamo wa Russia ni ama kuangamizwa au kutiwa mbaroni na kuhukumiwa. Pamoja na hayo Uturuki ambayo ni mwakilishi wa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani inataka kuyabakisha makundi ya kigaidi katika eneo hilo likiwemo genge la Tahriru sh-Sham ambalo awali lilijulikana kwa jina la 'Jabhatu Nusra' na ambalo ni tawi la mtandao wa Al-Qaidah nchini Syria.

Mbali na Russia, jeshi la Syria pia linatekeleza operesheni kali za kuwafyeka magaidi wanaosaidiwa na Uturuki, Marekani nk

Kundi hilo na kigaidi lina maelfu ya wapiganaji wa kigeni wanaotekeleza jinai nchini humo. Licha ya kwamba kundi la Jabhatu Nusra lilitajwa na Umoja wa Mataifa kuwa kundi la kigaidi, lakini serikali ya Ankara na hata Washington kwa pamoja zimeendelea kuliunga mkono wa hali na mali. Hakuna shaka kwamba lengo lao ni kuidhoofisha serikali ya Syria kupitia njia ya kuendelea uwepo wa harakati za makundi ya kigaidi ndani ya nchi hiyo na kuizuia serikali ya Damascus kudhibiti kikamilifu ardhi yake yote. Katika kipindi chote cha vita vya ndani nchini Syria, mrengo wa Magharibi na wa Kiarabu umekuwa ukifanya jitihada za kuyaokoa makundi ya kigaidi katika ardhi ya Syria kwa kutumia visingizio mbalimbali kama haki za binadamu mara zote makundi hayo yanapozidiwa nguvu na jeshi la Syria na waitifaki wake.  Hatua kama hii zinachukuliwa kwa shabaha ya kuyapunguzia mashinikizo makundi hayo ya kigaidi ya kuyapa fursa ya kujizatiti na kujijenga upya.

Wakati huo huo na kutokana na akthari ya magaidi yaliyopo Idlib kuwa na asili ya Russia, Caucasian na Asia ya Kati, viongozi wa ngazi ya juu wa Russia wana wasiwasi wa kurejea magaidi hao kwenye nchi hizo kutoka Syria na kuanza upya vitendo vya kigaidi. Ni kwa sababu hiyo ndio maana serikali ya Moscow inataka mapambano dhidi ya magaidi katika mkoa wa Idlib yaendelee hadi magaidi hao watakapomalizwa kabisa au wajisalimishe.

Tags

Maoni