Mar 19, 2020 07:28 UTC
  • Waislamu Uingereza wawasaidia wenye mahitaji wakati huu wa mripuko wa Corona

Waislamu nchini Uingereza, mijini na vijijini wanafanya jitihada za kukusanya bidhaa muhimu za msingi kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye mahitaji na wasiojiweza nchini humo, katika kipindi hiki cha mripuko wa Corona.

Mwandishi wa habari wa kanali ya televisheni ya Press TV mjini London ameripoti kuwa, Waislamu nchini Uingereza licha ya kuwa miongoni mwa jamii za walio wachache nchini humo, lakini wanafanya jitihada za kila aina kuwasaidia maskini na watu wenye mahitaji katika jamii wakati huu wa kupambana na Corona.

Makundi ya vijana wa Kiislamu nchini London yanakusanya vitu vya msingi vinavyohitajika kama chakula, karatasi za shashi (tishu) na sabuni za kuua viini kwa ajili ya kuwapa wasio na uwezo katika jamii za nchi hiyo ya Ulaya.

Baadhi ya Waislamu wenye maduka huko Scotland na hata mjini London wanawapa wenye kujitahi mfuko wenye bidhaa za msingi zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya Corona kama karatasi za shashi na sabuni za kuua vijidudu maradhi.

Wanawake Waislamu barani Ulaya

Harun Khan, Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu nchini Uingereza ambalo linasimamia misikiti na taasisi zaidi ya 500 za Kiislamu amesema Waislamu kama walivyo raia wengine katika jamii ya Uingereza, wanafanya jitihada za kupunguza maambukizi ya virusi vya corona sambamba na kundelea na shughuli zao za kila siku.

Takwimu za maambukizi ya virusi vya corona nchini Uingereza zinaongezeka siku baada ya nyingine na hadi sasa zaidi ya watu 1,963 wameambukizwa virusi hivyo na 71 miongoni mwao wameaga dunia. 

Tags

Maoni