Mar 25, 2020 07:01 UTC
  • Mwito wa wabunge wa Marekani wa kupunguzwa vikwazo vya nchi hiyo dhidi ya Iran

Baada ya serikai ya Trump huko Marekani kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei 2018, ilianza kuiwekea Iran vikwazo vya kila namna ambavyo Trump anajingamba kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kuwekewa vikwazo vikubwa, vikali na vingi kama alivyoiwekea Iran.

Jinai hiyo ya Marekani sasa hivi imesadifiana na kuenea kirusi hatari cha corona nchini Iran huku Washington ikishadidisha vikwazo vya kuzuia kufika Iran bidhaa na mahitaji ya dharura ya kupambana na corona. Hata hivyo si wanadamu wote wana nyoyo za jiwe, za kigaidi na za kikatili kama za Donald Trump na serikali yake. 

Sauti za kupinga vikwazo hivyo dhidi ya Iran leo hii zimezidi kusikika kote ulimwengu na hata ndani ya Marekani kwenyewe. Baada ya viongozi wa Iran na taasisi za kimataifa kulaani vikali vikwazo hivyo vya kidhulma, vya kigaidi na kikatili vya serikali ya Donald Trump sauti ya kupinga vikwazo hivyo hivi sasa inasikika kutoka ndani ya mabaraza ya kutunga sheria ya Marekani kwenyewe, yaani mabaraza Congress na Senate ambapo wabunge na maseneta wa nchi hiyo wameandika barua na kumtaka Trump apunguze vikwazo vyake dhidi ya Iran.

Jitihada za kupambana na kirusi cha corona nchini Iran. Hapa ni katika uzalishaji wa mada za kuua virusi

 

Katika barua yao hivyo, wabunge na maseneta hao wa Marekani wamesisitiza kuwa, mashinikizo makubwa ya White House yameathiri sekta za afya na mitababu nchini Iran. 

Katika barua yao hiyo, wabunge na maseneta wa Marekani wamegusia ripoti ya shirika la Human Rights Whatch ya mwaka 2019 kuhusu athari mbaya za vikwazo vya Marekani katika sekta ya afya na matibabu nchini Iran na kuandika: Vikwazo vya kiwango cha juu kabisa vya Marekani vimeusababishi matatizo makubwa uwezo wa mashirika ya Kiirani ya kudhamini fedha za kuingiza bidhaa na mahitaji ya kimsingi ya kibinadamu yakiwemo madawa muhimu mno na vifaa vya matibabu.

Aidha watunga sheria hao wa Marekani wamewaonya Mike Pompeo na Steven Mnuchin kwamba vikwazo vya Marekani vilivyolenga uchumi wa nchi nzima bila ya shaka yoyote vimesababisha matatizo katika juhudi za kudhamini mahitaji ya watu milioni 80 wa Iran na hicho ni kikwazo katika juhudi za kununua bidhaa za kimsingi tena wakati huu wa kuenea kirusi cha corona nchini Iran. Wabunge na maseneta hao wa Marekani wametilia mkazo wajibu wa kupunguzwa vikwazo katika sehemu kubwa ya uchumi wa Iran kama vile katika sekta ya uzalishaji wa bidhaa zisizo za kijeshi, mfumo wa benki na mauzo ya mafuta hadi mgogoro wa corona utakapomalizika kikamilifu.

Kuendelea vikwazo na mashinikizo ya kila upande ya Marekani dhidi ya Iran kumepelekea pia kuanza kuzungumziwa suala la "vikwazo vya kiwango cha juu vya Marekani dhidi ya mfumo wa afya na matibabu wa Iran." Ni jambo lisilo na shaka kwamba vikwazo vya kiwango cha juu kabisa vya serikali ya Trump dhidi ya Iran ni kikwazo katika jitihada za Tehran za kupambana vilivyo na maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19. 

Donald Trump, rais wa Marekani anayeshutumiwa kote duniani kwa ugaidi wa kiuchumi, kitiba na kisiasa

 

Ijapokuwa ukiuangalia mfumo wa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran utaona kuwa bidhaa muhimu za masuala ya kibinadamu hazijawekewa vikwazo rasmi, lakini wataalamu wa masuala ya vikwazo wanasema kuwa, ukweli wa jambo hilo ni tata sana. Bidhaa hizo hazikutajwa rasmi kuwa ni miongoni mwa mambo yaliyowekewa vikwazo, lakini njia zote za utekelezaji wake zimefungwa na vimewekwa chini ya masharti 12 yaliyotangazwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo. Katika matamshi yake ya hivi karibuni, Pompeo alidai kuwa bidhaa kama za madawa na chakula hazijawekewa vikwazo, lakini Iran haiwezi kupokea bidhaa hizo isipokuwa kupitia nchi ya tatu tena kwa sharti la kuwaachilia huru wafungwa wa nchi za kigeni walioko nchini Iran.

Tab'an kama tulivyosema huko nyuma, mwito wa kuitaka Marekani ipunguze vikwazo vyake dhidi ya Iran hautolewi na maseneta na wabunge wa nchi hiyo tu, bali mashirika 25 ya Marekani yakiwemo makundi ya haki za binadamu, vyuo na taasisi za misaada za nchi hiyo zimemwandikia barua Donald Trump na Wizara ya Mambo ya Nje na ile ya Hazina nchini humo kuitaka White House iangalie upya siasa zake kuhusu Iran kutokana na kuenea kirusi cha corona humu nchini.

Taasisi hizo zimemtaka Trump asimamishe vikwazo vyake dhidi ya Iran angalau kwa siku 120 vikiwemo vikwazo vya kifedha na mafuta pamoja na uzalishaji wa bidhaa zisizo za kijeshi. Hata hivyo licha ya kushinikizwa vyote hivyo, serikali ya Trump inaendelea kuonesha ukaidi na inazidi kuonesha sura yake ya kikatili na ukosefu wa utu dhidi ya wananchi wa Iran ambao wanahitajia sana vitu hivyo vya dharura katika wakati huu wa vita dhidi ya maambukizi ya kirusi cha corona yaani COVID-19.

Tags

Maoni