Mar 26, 2020 05:28 UTC
  • Hitilafu za kisiasa zaongezeka nchini Marekani kuhusu makabiliano na Corona

Kuenea virusi vya Corona na ugonjwa wa Covid-19 nchini Marekani si tu kwamba kumekuwa na taathira kubwa za kiuchumi na kijamii, bali pia kumegeuka na kuwa mjadala mkubwa ndani ya Bunge la Kongresi na ikulu ya White House.

Katika uwanja huo wabunge wa Kongresi wanaamini kuwa, ni lazima kuanze kutekelezwa hatua za haraka na za dharura katika kukabiliana na virusi vya Corona katika majimbo yote ya Marekani, huku kwa upande wake Rais Donald Trump wa nchi hiyo na kwa kuzingatia maslahi yake ya kisiasa na kiuchumi akisisitiza kuhitimishwa hatua za sasa za kupambana na Corona na badala yake kurejeshwe haraka hali ya ustawi wa kiuchumi nchini humo. Katika mkutano na waandishi wa habari ambao ulifanyika kwa njia ya mtandao wa kijamii ndani ya ikulu ya White House, Trump alitahadharisha juu ya kusimamishwa kwa muda mrefu shughuli za kiidara nchini humo na pia suala la karantini ya nyumbani kwa lengo la kukabiliana na virusi vya Corona. Alisema: "Nchi yoyote inaweza kusambaratika iwapo shughuli zake za kila siku zitasimamishwa. Mnapaswa kuchukua uamuzi. Sisi kila mwaka huwa tunapoteza maelfu ya watu kwa ugonjwa wa mafua. Hatufungi nchi. Ningependa tuendelee kusimamisha shughuli hadi Aprili 15 tu." Aidha akitumia takwimu za vifo vinavyosababishwa na ajali za barabarani na maradhi ya mafua nchini Marekani kwa mwaka, amesema kuwa takwimu hizo hazijapelekea kufungwa nchi. Kwa makusudi Trump amepuuza hatari isiyo ya kawaida inayotokana na virusi vya Corona na ugonjwa wa Covid-19 si tu kwa Marekani, bali kwa dunia nzima ambapo ameufananisha ugonjwa huo na matukio mengine ya kawaida kama vile ajali za barabarani. Suala hilo limewafanya wabunge wengi wa chama cha Democrat na Republican kutahadharisha juu ya uwezekano wa kuongezeka maambukizi ya virusi vya Corona nchini Marekani kutokana na msimamo wa Trump wa kupinga kuwekwa vizuizi katika sekta ya uchumi, biashara na viwanda. 

Trump asiyejali afya ya Wamarekani na badala yake kuzingatia maslahi ya kiuchumi na ushindi kwenye uchaguzi wa 2020

Lindsey Graham, Seneta wa ngazi ya juu wa chama cha Republican ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter juu ya Trump kutokuwa na nia thabiti ya kupambana  na Corona. Viongozi wengine wa ngazi za juu katika bunge la Kongresi pia wametoa maoni kama hayo kuhusiana na suala hilo. Nancy Pelosi, Spika wa Bunge la Kongresi la Marekani alisema hivi karibuni katika mahojiano: "Gharama za kiuchumi za watu waliodhurika na ugonjwa, ni kubwa zaidi ya hivi tunavyoshuhudia." Wakosoaji wa serikali ya Trump wanaamini kwamba jambo linalopewa umuhimu wa kwanza na rais huyo ni maslahi yake binafsi ya kiuchumi na kisiasa, suala ambalo ni kinyume na msimamo na nara yake ya 'Marekani Kwanza.' Suala hilo linashuhudiwa zaidi katika mwenendo wake kuhusiana na Corona. Licha ya wasiwasi mkubwa uliopo kuwa huenda uzembe wa serikali ya Trump kuhusiana na Corona, ukapelekea zaidi ya watu milioni mbili nchini humo kuwa wahanga wa virusi vya Corona na kusababisha mdororo mkubwa katika uchumi wa nchi hiyo, lakini Trump asiyejali lolote amepuuzilia mbali wasiwasi huo na kutaka shughuli za nchi hiyo zirejee katika hali ya kawaida haraka iwezekanavyo. Ukweli ni kwamba kitendo cha rais huyo mwenye kashfa nyingi cha kujiepusha kutekeleza hatua ambazo alitakiwa kuzichukua, kitamfanya kuwa mbeba dhima ya maafa ya kibinaadamu na kuongezeka kwa mdororo wa uchumi wa nchi hiyo. Trump anadhani kwamba ataweza kuizuia Marekani kukumbwa na mporomoko mkubwa wa kiuchumi.

Virusi vya Corona, tishio kubwa kwa Marekani

Hii ni kusema kuwa, inatabiriwa kwamba katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu wa 2020, Marekani itaingia katika mporomoko mkubwa wa kiuchumi ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia yake. Kuthibiti utabiri huo kuna maana ya kutoweka mafanikio ya kiuchumi yanayodaiwa na Trump, yaani kusambaratika ndoto yake muhimu ya kumuwezesha kushinda uchaguzi wa mwaka huu. Kuhusiana na suala hilo Stephen K. Bannon, mtaalamu wa zamani wa stratijia katika ikulu ya Marekani amesema: "Katika uchaguzi wa rais wa 2020 Trump atalazimika kupambana na virusi vya Corona badala ya kuchuana na wagombea wa Democrat." Akisisitizia ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona na taathira yake mbaya ambayo ni tishio kwa Marekani Bannon amesema: "Trump asichuane na Joe Biden, bali anatakiwa apambane na virusi hivi na madhara yanayotokana navyo. Wamarekani watampima Trump kwa msingi wa alivyopambana na mgogoro huu." Kwa utaratibu huo, tunaweza kusema kuwa Trump kinyume na wanavyotaka wabunge wa Baraza la Kongresi kuhusu kuchukuliwa hatua pana zaidi na za dhati za kukabiliana na Corona, anataka kuzuia hatua hizo. Suala muhimu ni kwamba Wamarekani wanapaswa kutoa radiamali kali dhidi ya mienendo isiyo sahihi ya Trump kuhusiana na virusi vya Corona vinavyoendelea kuhatarisha maisha yao.

Tags

Maoni