Mar 26, 2020 08:02 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN: Kirusi cha corona ni tishio kwa 'binadamu wote kwa ujumla wao'

Katbu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezindua kampeni ya ombi la kuchangia dola bilioni mbili za msaada wa kimataifa wa huduma za kibinadamu kwa ajili ya nchi zilizo masikini zaidi ili kuziwezesha kupambana na janga la kirusi cha corona, huku idadi ya vifo vinavyosababishwa na kirusi hicho katika nchi za Italia na Uhispania ikizidi kuongezeka.

Antonio Guterres amesema, COVID-19 ni tishio kwa binadamu wote kwa ujumla, hivyo wanadamu wote kwa ujumla wao wanapaswa kupambana na kukabiliana na tishio hilo.

Guterres amezindua kampeni hiyo huku vifo zaidi vikiripotiwa barani Ulaya na kulifanya eneo hilo kuwa kitovu cha mripuko wa kirusi hicho angamizi. Uhispania imeripoti vifo vya zaidi ya watu 700 katika muda wa saa 24 zilizopita na kuifanya nchi ya pili duniani baada ya Italia iliyoathiriwa vibaya zaidi na Covid-19.

Katika hotuba yake kwenye uzinduzi wa ombi hilo, Katibu Mkuu wa UN amesema, nchi masikini zaidi duniani ni zile zenye mifumo duni ya afya, ambako watu waliofurushwa makwao kwa sababu ya mabomu, ghasia na mafuriko, wanaishi kwenye nyumba zilizoezekwa kwa karatasi za plastiki au wamerundikana kwenye kambi za wakimbizi au makazi yasiyo rasmi.

Watu wanaoishi katika mazingira duni ya ukimbizi wanakabiliwa na tishio kubwa la maambukizi ya covid-19

“Watu hawa hawana nyumba au makazi, ambamo kwamo wanaweza kujitenga na wengine ili kuepusha maambukizi ya virusi vya Corona,” amesema Guterres.

Hata hivyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, endapo fedha hizo zinazoombwa zitapatikana lakini zikatumiwa ndivyo sivyo, itakuwa ni janga, kwa sababu “kipindupindu kitasambaa na surua, homa ya uti wa mgongo na viwango vya utapiamlo vitaongezeka, na hivyo kufutilia mbali uwezo wa mataifa hayo kukabiliana na virusi vya Corona.”

Ameongeza kuwa, kuunga mkono ombi hilo ni muhimu kwa ajili ya kulinda afya duniani na ni jambo la kimaadili na ni kwa maslahi ya kila mkazi wa dunia.

Katibu Mkuu wa UN ametoa wito pia kwa serikali kuliunga mkono ombi hilo akikumbusha kuwa, wakati nchi tajiri nazo zinahaha kukabili virusi, katika nchi zilizo masikini, ambako hata mifumo ya afya ni dhaifu, huduma za kujikinga na Corona kwa kunawa mikono na sabuni, bado ni changamoto kubwa.../

Tags

Maoni