Mar 26, 2020 12:52 UTC
  • Corona na kushadidi changamoto za kiuchumi barani Ulaya

Kugeuka Ulaya na kuwa kitovu cha kuenea virusi vya Corona (Covid-19) katika siku siku za hivi karibuni sambamba na kuongezeka idadi ya walioambukiizwa na virusi hivyo barani Ulaya kumepelekea kuibuka wasiwasi mkubwa katika uga wa utoaji huduma za tiba, afya, huduma za kibinadamu na kijamii katika nchi za bara hilo.

Sambamba na kipindi hiki cha kufanyika juhudi za kudhibiti maradhi hayo, kumeongezeka wasiwasi wa taathira hasi na za muda mrefu kwa uchumi na siasa barani humo.

Kufungwa mipaka, kuweko sheria kali za kutembea, kufungwa sekta ya viwanda na kusimamisha shughuli zake akthari ya mashirika ya ndege ni mambo ambayo yamewafanya viongozi wengi barani Ulaya watoe indhari kuhusiana na kudorora uchumi mara baada ya kupita kipindi hiki cha virusi vya Corona na kuwafanya wafikirie mikakati ya kuja kukabiliana na hali hiyo hapo baadaye. Ursula von der Leyen, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya ameashiria matokeo mabaya kwa uchumi kutokana na kuenea virusi vya Corona na kusema kuwa: Ili sisi tukabiliane na virusi hivi tunapaswa kudhibiti kwa namna fulani maisha yetu ya kawaida, hata hivyo jambo hili linatoa pigo kwa uchumi wetu.

Bendera ya Umoja wa Ulaya

Utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa, sehemu kubwa ya uchumi wa eneo la Euro imesimama kwa muda kutokana na taathira ya kila upande ya virusi vya Corona, jambo ambalo litatoa pigo kubwa kwa shughuli za kiuchumi katika eneo hilo. Kadhalika uchumi wa Umoja wa Ulaya katika mwaka huu wa 2020 ambao ulitabiriwa kuongezeka kwa asilimia 4.1 utapungua kwa asilimia moja kutokana na maradhi ya Covid-19.

Ujerumani na Ufaransa nchi mbili kuu za Ulaya ambazo zina nafasi muhimu katika uchumi wa Bara Ulaya, filihali zinakabiliwa na hali ya chumi zao kudorora. Makadirio yanaonyesha kuwa, hasara itakayosababishwa na virusi vya Corona katika kipindi cha miezi miwili hadi mitatu kwa uchumi wa Ujerumani itafikia Euro bilioni 255 hadi 497; na endapo hali hiyo itaendelea kwa muda wa miezi mitatu hasara itakayosababishwa na virusi hivyo kwa uchumi wa nchi hiyo kubwa kiviwanda barani Ulaya inakadiriwa kufikia Euro bilioni 354 hadi 729.

Maelekezo ya kujikinga na viruso vya Coro9na

Weledi wa mambo wanasema kuwa, kupotea nafasi milioni moja za ajira na kuporomoka uchumi kwa asilimia 20 ni matokeo mengine hasi ya Corona kwa uchumi wa Ujerumani. Vile vile inaelezwa kuwa, uzalishaji wa bidhaa ghafi nchini Ufaransa kwa sasa umepungua kwa asilimia 20.

Hii ni katika hali ambayo, kabla ya hapo nchi mbalimbali za Umoja wa Ulaya zilikuwa zikikabiliwa na matokeo mabaya ya kisiasa na kiuchumi ya kujiondoa Uingereza katika umoja huo (Brexit), kuongezeka ukosefu wa ajira, malalamiko ya kijamii yanayotokana na marekebisho ya sheria za ulipaji kodi na kustaafu bila kusahau jinamizi la mgogoro wa wahajiri.

Hivi sasa kuibuka virusi vya Corona kumeshadidisha zaidi matatizo ya nchi za Umoja wa Ulaya kiasi kwamba, kuna wasiwasi kuwa, matatizo ya kiuchumi huenda yakawa na taathira mbaya kwa umoja wa eneo la Euro pamoja na siasa za pande kadhaa za umoja huo.

Bruno Le Marie, Waziri wa Uchumi wa Ufaransa ametahadharisha kwamba: Mgogoro wa virusi vya Corona unatishia hata uwepo wa eneo la Euro na unatilia alama ya swali mustakabali wa kisiasa wa Bara la Ulaya; ni kwa msingi huo ndio maana ima eneo la Euro lionyeshe radiamali ya pamoja dhidi ya mgogoro wa kiuchumi na kufanikiwa kuvuka mgogoro mkubwa zaidi ya huu au kila nchi miongoni mwa nchi za eneo hilo ionyeshe radiamali kivyake na hivyo eneo hilo likabiliwe na hatari ya kusambaratika.

Hivi sasa viongozi mbalimbali wa Ulaya wamo mbioni kuandaa mbinu na kustafidi na mikakati mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na mgogoro mkubwa zaidi wa kiuchumi utakaosababishwa na virusi vya Corona. Pamoja na hayo, endapo hali hii itaendelea na kukaweko hatua za upande mmoja, kukakosekana ushirikiano baina ya nchi za Ulaya na kutofungamana kwao na uchukuaji hatua kwa pamoja, kutalifanya suala la umoja na mshikamano wa Umoja wa Ulaya kukabiliwa na hatari.

Tags