Apr 01, 2020 09:41 UTC
  • Wasi wasi wa Umoja wa Ulaya kuhusu kuendelea mapigano nchini Yemen, undumakuwili wa EU

Tangu mwezi Machi 2015, Saudi Arabia iliunda muungano kwa kushirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kuanzisha vita vya kidhalimu dhidi ya watu wa Yemen na hadi sasa makumi ya maelfu ya raia wa nchi hiyo wameshauawa shahidi na kujeruhiwa.

Baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani zimekuwa na mchango mkubwa katika vita hivyo kupitia aina mbalimbali za misaada ya kilojestiki, kutoa taarifa za kijasusi na kuwaunga mkono Wasaudia na Waimarati. katika jinai wanazofanya huko Yemen. Kufuatia mashambulizi mapya ya muungano vamizi wa Saudia nchini Yemen hususan katika hujuma za muungano huo kwenye miji tofauti ya nchi hiyo ya Kiarabu, siku ya Jumatatu wiki hii, Umoja wa Ulaya ulitoa taarifa ya kudai inasikitishwa na ukiukwaji wa usitishaji vita nchini Yemen. Taarifa hiyo iliyosomwa na msemaji wa Umoja wa Ulaya imesema: "Licha ya mapendekezo ya mara kadhaa ya jamii ya kimataifa kwa pande za mapigano nchini Yemen kutekeleza agizo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na usitishaji vita, lakini bado mapigano ya kijeshi yangali yanaendelea." Msemaji wa Umoja wa Ulaya amemsisitizia Martin Griffith, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, udharura wa kusimamishwa haraka mapigano ya silaha nchini humo. Aidha umoja huo umezitaka pande husika za mapigano kustafidi na fursa iliyopatikana kwa ajili ya kupunguza vita na kutumia fursa hiyo kutangaza rasmi usitishaji vita baina yao. Kadhalika Umoja wa Ulaya umesisitiza kuwa utaendelea na uungaji mkono wake kamili kwa mwenendo uliochukuliwa na Umoja wa Mataifa.

Licha ya jinai kubwa za kinyama zinazofanywa na Saudia, lakini Umoja wa Ulaya (EU) umeendelea kuwa na misimamo ya kiundumakuwili

Taarifa hiyo imetolewa wakati ambao hadi sasa Umoja wa Ulaya (EU) haujatilia maanani hata kidogo hatua za uharibifu za muungano vamizi wa Saudia katika kuendeleza vita vyake vya kidhalimu dhidi ya raia madhlumu wa Yemen, licha ya kwamba muungano huo vamizi umeendelea kukanyaga mapatano ya hivi sasa kuhusu usitishaji vita, na unaendeleza mashambulizi yake katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ya Kiislamu. Umoja wa Ulaya umedai kwamba mashambulizi ya makombora ya Harakati ya Answarullah nchini Saudi Arabia na pia mapigano ya kijeshi katika mkoa wa Ma'rib na viunga vyake, na vilevile mashambulizi ya hivi karibuni katika mkoa wa Sana'a yaliyofanywa na ndege za Saudia, yameutia wasi wasi mkubwa umoja huo. Pamoja na hayo wanachama wa umoja huo hawakutilia maanani suala hili kwamba operesheni za muqawama wa Yemen ikiwemo kuvurumisha makombora na pia operesheni zake za ndege zisizo na rubani dhidi ya utawala wa Aal Saud, ni radiamali tu kufuatia hatua za kivamizi na zisizo za kibinaadamu za Wasaudia na Waimarati dhidi ya raia madhlumu wa Yemen. Wanachama hao wa EU wanauchukulia mgogoro wa Yemen kwa namna ambayo wanajaribu kuonyesha kwamba ni Wayemen ndio walioanzisha uchokozi na vita dhidi ya Saudia na Imarati, jambo ambalo si sahihi hata kidogo. Suala jingine ni kwamba, wakati Umoja wa Ulaya unataka usitishaji vita nchini Yemen, baadhi ya nchi za umoja huo kama vile Ufaransa, Uingereza kwa kushirikiana na Ujerumani zinaendelea kupuuza suala la kuacha kuuzatiti muungano vamizi wa Saudia kwa kuziuzia silaha nyingi Saudi Arabia na Imarati. Ni kutokana na upinzani wa vyama vya mrengo wa kushoto, ndipo serikali ya muungano nchini Ujerumani imelazimika kusitisha kwa mara ya tatu uuzaji wa silaha kwa utawala wa Saudia, hata hivyo Ufaransa kama nchi muhimu ya pili katika Umoja wa Ulaya, ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu kwa muungano vamizi wa Saudia katika vita nchini Yemen. Ufaransa kama nchi ya tatu kubwa muuzaji wa silaha kwa Saudi Arabia sawa na Marekani na Uingereza, ina nafasi kubwa katika kuunga mkono muungano vamizi wa Saudia.

Josep Borell, Mkuu Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya

Hii ni kusema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Paris na Riyadh zimezidisha mno ushirikiano wao wa kijeshi na silaha na katika uwanja huo, matokeo ya safari ya Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia hapo mwanzoni mwa mwezi Aprili 2018 nchini Ufaransa, alitiliana saini mikataba ya kijeshi na kiuchumi yenye thamani ya dola bilioni 18. Mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana, Mohammed Ali al-Houthi, Mkuu wa Baraza Kuu la Mapinduzi nchini Yemen sambamba na kubainisha kwamba Ufaransa inaipatia Saudia uwezo wake wa kijeshi na silaha, alisema kuwa hiyo ni jinai, na kwamba hatua ya serikali ya Paris kutiliana saini mikataba ya silaha na nchi zinazoishambulia Yemen na kuwatumia silaha wavamizi hao, inakwenda kinyume na katiba ya Ufaransa. Hata kama Uingereza pia tarehe 31 Januari mwaka huu ilijiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, lakini katika miaka ya hivi karibuni ilikuwa ni mdhamini mkubwa wa silaha kwa Saudia. Tarehe 29 Machi mwaka huu gazeti la Uingereza la The Guardian lilitoa ripoti ambayo ilionyesha kwamba tangu mwaka 2015 Saudia imenunua silaha za takriban Pauni milioni 5.3 ambazo ni sawa na dola bilioni sita kutokakwa Uingereza. Kwa mujibu wa Andrew Smith, Msemaji wa Taasisi Inayopinga Biashara za Silaha; silaha za Uingereza nchini Yemen ndicho kichocheo kikuu cha kuendelea vita ndani ya nchi hiyo. Miamala hiyo ya silaha, ni kinyume na maadili kama ambavyo pia ni kinyume na uamuzi wa mahakama na sheria. Ukweli ni kwamba iwapo Umoja wa Ulaya una nia ya kweli ya kusitishwa vita nchini Yemen, kwanza unatakiwa kujiepusha na tabia yake ya kuendeleza mauzo ya silaha kwa wavamizi wa Yemen yaani Saudia na Imarati.

Tags

Maoni