Apr 04, 2020 04:13 UTC
  • Madai ya uongo ya Trump kuwa eti Iran haijaomba kupunguziwa vikwazo

Baada ya kujitoa bila ya sababu katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei 2018 serikali ya Donald Trump huko Marekani iliirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo, bali iiiwekea Tehran vikwazo vya kiwango cha juu kabisa kama anavyojitapa mara kwa mara Donald Trump.

Vikwazo vikubwa vya Marekani vimeongezwa hata baada ya takriban nchi zote duniani ikiwemo Iran kukumbwa na ugonjwa wa COVID-19. Hatua hiyo imeamsha hisia za walimwengu waliozidi kuona ugaidi wa kiuchumi na kimatibabu wa Donald Trump na wenzake. Radiamali za Tehran na taasisi nyingi za kimataifa pamoja na baadhi ya nchi duniani zimeiweka chini ya mashinikizo makubwa Marekani na kumfanya Donald Trump akimbilie kusema uongo ili kupunguza mashinikizo hayo.

Lakini si jambo la kushangaza kumuona Trump anasema uongo kuhusu suala hilo kwani rais huyo wa Marekani amevunja rekodi zote za kusema uongo. Akizungumza mbele ya waandishi wa habari na katika kujibu swali kuhusu Marekani kupunguza vikwazo vyake dhidi ya Iran katika kipindi hiki cha kuenea kirusi cha corona, Trump alidai kwamba: Uchumi na jeshi la Iran vimepata pigo kubwa na kirusi cha corona nacho kimeisababisha madhara makubwa nchini Iran. Jamhuri ya Kiislamu haijatoa ombi lolote la kupunguziwa vikwazo ili kuruhusu kutumwa vifaa vya matibabu nchini humo. 

Dk Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

 

Trump amesema uongo huo hadharani na bila ya kiwewe katika hali ambayo, tayari Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeuomba rasmi Umoja wa Mataifa ukomeshe vikwazo visivyo na chembe ya ubinadamu vya Marekani dhidi ya Iran ili kwa njia hiyo uweze kuruhusu mapambano dhidi ya corona yafanyike kwa ufanisi nchini Iran. Tarehe 12 Mchi 2020, Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, na nakala ya barua hiyo aliitumia kwa wakuu wa taasisi zote za kimataifa pamoja na mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa nchi za dunia akitaka kukomeshwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran kwani vikwazo hivyo ni kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 humu nchini. Katika barua hiyo, Zarif alitaka kukomeshwa mara moja ugaidi wa kiuchumi na kimatibabu wa serikali ya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran na kuutaka Umoja wa Mataifa na nchi wanachama wake kutekeleza majukumu yao ya kibinadamu ya kuwaunga mkono wananchi na serikali ya Iran katika kuilazimisha Marekani ikomeshe vikwazo vyake. Vile vile alimuomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aifanye barua yake hiyo kuwa ni ushahidi mbele ya Baraza Kuu na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Katika sehemu moja ya barua hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliandika: Licha ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na uwezo mkubwa wa kielimu na licha ya kwamba inawajibika ipasavyo katika kupambana na maambukizi ya kirusi cha corona, lakini vikwazo vya Marekani na masharti yaliyowekwa hivi karibuni na viongozi wa nchi hiyo ni kizuizi katika mauzaji na manunuzi ya dawa na vifaa vya matibabu pamoja na misaada ya kibinadamu kwa Iran suala ambalo linakwamisha sana  jitihada za kupambana na ugonjwa wa COVID-19 humu nchini. 

Licha ya kuweko ugaidi wa kimatibabu na uadui wa Marekani inayozuia vifaa vya tiba kuingia nchini Iran, lakini taifa la Iran limeazimia kikwelikweli kupambana na COVID-19 na hadi sasa limepata mafanikio katika jitihada zake hizo

 

Inavyoonekana ni kuwa Donald Trump alikuwa anaota kwamba Iran itawasiliana moja kwa moja na Marekani na kuomba msaada. Trump alishindwa kuficha ndoto yake hiyo ya muda mrefu aliposema mbele ya waandishi wa habari kwamba: Jambo pekee wanalopaswa kufanya Wairani ni kutupigia simu na kutuomba msaada. Lakini Trump anasema uongo hata katika madai yake haya, kwani kabla ya hapo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo, alishurutisha suala la kuachiliwa huru wafungwa wa kigeni nchini Iran na suala la kuruhusu Marekani kufika misaada ya kibinadamu humu nchini. Lakini Iran imetangaza wazi tangu zamani kwamba haiko tayari kufanya mazungumzo na Marekani na kwamba hatua ya Iran ya kumwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kumtaka ailazimishe Marekani ikomeshe vikwazo vyake vya kidhulma na kigaidi dhidi ya wananchi wa Iran, ni ushahiwidi wa wazi kwamba njozi ya Trump ya kufanya mazungumzo na Iran haitotimia na itaendelea kuwa ndoto ya alinacha tu.

Kwa kweli siasa za kiuadui za Donald Trump dhidi ya Iran ni za kuchupa mipaka na haziingii akilini kiasi kwamba hata baadhi ya watawala wa Marekani pamoja na Baraza la Congress la nchi hiyo wanaukiri uhakika huo. Pamoja na hayo hakuna dalili zozote zinazoonesha kwamba kuna siku Trump atabadilisha misimamo yake ya kiuadui dhidi ya Iran. Ukweli ni kuwa Trump si tu hana msaada wowote kwa Iran, bali katika siku za hivi karibuni amezidi kuonesha chuki zake kwa kutoa vitisho vipya dhidi ya Tehran na wala wananchi wa Iran hawana haja na msaada wake.

Tags

Maoni