Apr 05, 2020 03:17 UTC
  • Ayatullah Alireza Arafi
    Ayatullah Alireza Arafi

Mkuu wa vyuo vya kidini katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemuandikia barua Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, na kusema vyuo vya kidini Iran viko tayari kubadilishana uzoefu na vyuo vya kidini na viongozi wa dini za mbinguni kote duniani.

Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran, IRNA, Ayatullah Alireza Arafi, mkurugenzi wa vyuo vya kidini Iran amemuandikia barua Papa Francis na kutangaza kufungamana na watu wa dini zote na mataifa yote ambao wamepatwa na msiba na kuathiriwa na ugonjwa wa corona.

Katika barua yake, Ayatullah Arafi ameongeza kuwa: "Katika mantiki ya dini za mbinguni, maafa na balaa za kimaumbile ni mtihani ambao huandaa mazingira ya kukamilika mwanadamu na fursa ya kustawi na kunawiri moyo wa mshikamano na kujitolea."

Aidha Mkuu wa vyuo vya kidini katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika barua hiyo kuhusu udharura wa kuimarishwa misingi ya kiitikadi na kuzingatia utakasaji wa nafsi na roho pamoja na kuilinda jamii ili isikumbwe na machafu au maovu. Pia ameashiria uwezo wa milele wa Mwenyezi Mungu SWT na kukumbusha kuwa: "Kukabiliana na changamoto iliyopo na migogoro mingine ya zama za sasa kama vile ukosefu wa uadilifu, vikwazo vilivyo dhidi ya binadamu, mgogoro wa mazingira, vita, na ugaidi yote yanahitaji kutafakari pamoja na ushirikiano wa kimataifa."

Papa Francis

Ameongeza kuwa kuna ulazima wa ushirikiano wa pande zote katika kukabiliana na sera zisizo za uwajibikaji za baadhi ya nchi za kibeberu na zile zinazochukua maamuzi ya upande mmoja. Hali kadhalika katika barua yake hiyo kwa Papa Francis, Ayatullah Arafi ametoa wito wa kuimarishwa msingi wa upendo, uadilifu, amani na mshikamano wa wanaadamu.

Ayatullah Arafi ameongeza kuwa: "Vyuo vya kidini vya Iran viko tayari kubadilishana uzoefu wa kielimu, kiutafiti, na utoaji misaada hasa katika uga wa intaneti. Amesema kwa njia hiyo kutafunguliwa ukurasa mpya wa kutafakari kwa pamoja na kushirikiana na taasisi za kielimu za kimataifa, vyuo  vikuu,  vituo vya kidini, viongozi wa dini za mbinguni, nchi za dunia na taasisi za Kikatoliki ili kuunda jamii moja ya dini za mbinguni kwa ajili ya kuhudumia jamii ya mwanadamu.

Tags

Maoni