Apr 05, 2020 08:03 UTC
  • Trump awataka Wamarekani wajiandae kwa 'vifo vingi' vya corona

Rais Donald Trump wa Marekani ameonya kuwa, taifa hilo litashuhudia vifo vingi vya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona ndani ya wiki mbili zijazo, huku nchi hiyo ikiendelea kuongoza kwa idadi ya watu walioambukizwa virusi hivyo duniani.

Akiongea na waandishi wa habari jana Jumamosi katika Ikulu ya White House, Trump alisema, "wiki hii itakuwa mbaya zaidi, na kwa bahati mbaya vifo vingi vitashuhudiwa baina ya wiki hii na wiki ijayo."

Rais huyo wa Marekani ameongeza kuwa, 'hatujahawahi kushuhudia kitu cha namna hii, na idadi hii kubwa (ya vifo) labda (vilishuhudiwa) tu katika vita, vita vya kwanza au vya pili vya dunia."

Hata hivyo Trump amedai kuwa baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vinaeneza woga na taharuki kwa kutangaza 'idadi kubwa zaidi' ya wahanga wa corona.

Corona yaifanya Marekani iibe maski za Wajerumani zilizokuwa zinatokea China

Kwa mujibu wa takwimu za Chuo Kikuu cha Johns-Hopkins, zaidi ya watu 8,000 wamefariki dunia nchini Marekani kwa sababu ya janga la Corona, ambapo zaidi ya watu 300,000 nchini humo wameambukizwa virusi hivyo.

Hivi karibuni, Ikulu ya White House ilitangaza kuwa, ugonjwa wa Covid-19 huenda utaua Wamarekani hadi laki mbili na elfu arubaini (240,000) ndani ya wiki mbili zijazo.

Tags

Maoni