Apr 05, 2020 11:49 UTC
  • Henry Kissinger
    Henry Kissinger

Waziri wa zamani wa Marekani, Henry Kissinger, amesema katika makala yake iliyochapishwa kwenye gazeti la The Wall Street Journal kwamba, mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona utabadilisha mfumo wa dunia milele.

Kissinger amesema madhara yaliyosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona kwa afya ya siha huwenda yakawa ya muda mfupi lakini machafuko na mtikisiko wake wa kisiasa na kijamii yumkini vikaendelea kushuhudiwa katika vizazi kadhaa vijavyo.

Amesema hali isiyo ya kawaida inayotawala dunia ya sasa inamkumbusha hisia alizokuwa nazo alipokuwa mwanajeshi katika kikosi cha nchi kavu wakati wa Vita vya Pili vya Dunia mwishoni mwa mwaka 1944, kwa sababu ya hisia za kukumbwa na hatari kubwa zinazotawala, hatari ambayo hailengi mtu binafsi pekee bali wanadamu wote na kwa sura ya kutisha na kuangamiza.

Kissinger amesema: "Licha ya mfanano uliopo baina ya kipindi hicho na hiki cha sasa, kuna tofauti kubwa ambayo ni uwezo wa Wamarekani wa kustahamili katika kipindi kile cha Vita vya Pili ulioimarishwa zaidi na juhudi za kutimiza malengo ya kitaifa, tofauti na wakati huu ambapo virusi vya corona vimeivamia Marekani iliyogawanyika kisiasa na inayotawaliwa na serikali isiyofaa na isiyo na muono wa mbali unaoiwezeha kushinda mashaka makubwa ya kimataifa yanayosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona.”

Henry Kissinger na Trump

Henry Kissinger pia amewakosoa viongozi wa nchi mbalimbali duniani akisema wanakabiliana na mgogoro wa sasa wa virusi vya corona kwa misingi ya utaifa japokuwa virusi hivyo havitambui mikapa ya nchi.

Amesisitiza kuwa hakuna nchi yoyote, hata Marekani, inayoweza kushinda mapambano ya virusi vya corona peke yake na kwa jitihada za kitaifa pekee, na kusema kuna udharura wa kuwepo ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo.

Kissinger amesema hayo huko Wamarekani wakiendelea kukosoa utendaji dhaifu wa Rais Donald Trump na serikali yake katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.

Marekani kwa sasa inaongoza kati ya nchi zilizoathiriwa sana na virusi vya corona na zaidi ya Warekani 288,35 wameambukizwa virusi hivyo. Siku ya jana pekee Wamarekani karibu 1,500 waliaga dunia kutokana na maambukizi ya corona.

Tags

Maoni