Apr 05, 2020 16:21 UTC
  • Trump: Wiki ijayo hali itakuwa mbaya zaidi Marekani na watu wengi watafariki dunia

Hali ya mambo nchini Marekani inazidi kuwa mbaya siku hadi siku kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya waathirika wa virusi vya Corona ambapo Rais Donald Trump wa nchi hiyo ametahadharisha kuhusu kuharibika hali ya mambo nchini.

Katika uwanja huo kanali ya televisheni ya CNN ya Marekani imeripoti kwamba, sambamba na kuongezeka idadi ya waathirika wa Corona na uhaba mkubwa wa nyenzo na vifaa vya tiba nchini humo, Rais Donald Trump ametahadharisha kuwa serikali yake inaamini kuwa, katika kipindi cha wiki moja ijayo hali ya mambo inatazamiwa kuwa mbaya zaidi huku watu wengi pia wakipoteza maisha. Hii ni katika hali ambayo Andrew Cuomo, gavana wa jimbo la New York naye ameonya kuwa vifaa vya kupumulia vilivyo katika hospitali za jimbo hilo, vinatosha kukidhi mahitaji ya wiki moja pekee na kwamba New York inahitajia vifaa zaidi kwa ajili ya wagonjwa wa Corona.

Corona iliyotapakaa kila kona nchini Marekani

Kadhalika zaidi ya polisi 1600 yaani karibu asilimia 18 ya maafisa usalama wa New York pamoja na maelfu ya wakazi wa mji huo, tayari wameathirika na virusi vya Corona. Mbali na hayo idara ya polisi ya mji huo imepoteza makumi ya maafisa wake kutokana na maradhi hayo. Aidha ikulu ya White House imeyataja majimbo mawili ya Wisconsin na Nebraska kuwa maeneo yenye maafa zaidi kutokana na idadi kubwa ya waathirika wa ugonjwa wa Covid-19 na kusisitiza kuwa, majimbo hayo yanahitaji misaada zaidi. Kwa mujibu wa takwimu za mwisho za wagonjwa wa Corona nchini Marekani, jumla ya watu laki tatu na elfu 11m,637 wameathirika virusi hivyo, huku wengine 8,454 wakiwa wamefariki dunia hadi sasa.

Tags

Maoni