Apr 06, 2020 02:31 UTC
  • Mzozo mpya katika uhusiano wa Uturuki na Ugiriki

Harakati mpya za viongozi wa Ankara na Athens, kwa mara nyingine zimechochea mizozo kati ya Uturuki na Ugiriki.

Hami Aksoy, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ametoa radiamali kufuatia hatua ya hivi karibuni ya Ugiriki kwa kusema kuwa, pendekezo la Waziri Mkuu wa nchi hiyo jirani kwa Ufaransa na Ujerumani ni mbaya sana na lisilo la kiakhlaqi. Amesisitiza kuwa hadi sasa Uturuki bado inawahifadhi wahajiri milioni nne kama wageni, huku ikiwa imetumia kiasi cha dola bilioni 40. Amesema, hata hivyo fikra za walio wengi duniani, hazijasahau miamala isiyo ya kibinaadamu na ya fedheha ya serikali ya Ugiriki kuwahusu wahajiri. Kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa Ugiriki sambamba na kutuma barua kwa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani aliwataka viongozi wa Umoja wa Ulaya kuiwekea masharti misaada ya kifedha inayotumwa Uturuki. Hali hiyo inaendelea katika hali ambayo duru nyingi za kisiasa zimezitaja hatua za hivi karibuni za serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki kuwa ni tishio kwa usalama na amani ya eneo na dunia. Katika uwanja huo, akthari ya weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba rais huyo wa Uturuki anatumia suala la wahajiri kama muhimili mkuu wa mashinikizo kwa ajili ya kuvutia uungaji mkono wa nchi za Magharibi kuhusu siasa za nchi yake nchini Syria. Aidha wataalamu wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa: "Serikali ya Ankara haipasi kutumia suala la wakimbizi na wahajiri kama wenzo na muhimili wa mashinikizo." 

Hami Aksoy, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki

Pamoja na hayo, inaonekana kuwa suala la wahajiri halitohitimisha mizozo iliyopo kati ya Uturuki na Ugiriki hivi karibuni. Ukweli ni kwamba, madamu usalama wa Syria haujapatikana na kuendelea wimbi la wahajiri wa nchi hiyo kuingia Uturuki, huku serikali ya Ankara ikiendelea pia kutumia suala la wahajiri kama wenzo wa mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi kwa nchi za Magharibi, kuna uwezekano wa mwenendo huo kubadilika na kuwa moja ya mizozo mikubwa kati ya pande hizo. Hii ni katika hali ambayo akthari ya weledi wa mambo wanasema kuwa makubaliano ya Uturuki na Umoja wa Ulaya yamekuwa na matunda na kuhusiana na suala hilo wanaamini kuwa makubaliano ya mwaka 2016 kati ya pande mbili yaliweza kufikia malengo yaliyokusudiwa. Kwa mfano, Gerald Knaus mtaalamu wa masuala ya uhajiri na mwanasaikolojia ambaye anatajwa kuwa mbunifu wa makubaliano ya Uturuki na Umoja wa Ulaya kuhusiana na kadhia ya wahajiri anaamini kwamba: "Hadi sasa makubaliano hayo yamefikia malengo yake." Akizungumza na mtandao mmoja wa habari wa nchini Ujerumani, mtaalamu huyo wa masuala ya wahajiri amesema: "Tangu mapatano kati ya Uturuki na Ulaya yatekelezwe, ni sehemu ndogo tu ya wakimbizi wa Syria ndio wameweza kuingia Ulaya kutokea Uturuki." 

Wakimbizi na wahajiri wanatumiwa na Uturuki kama chombo cha kuzishinikiza nchi za Ulaya

Akizungumzia tofauti kati ya pande mbili za Uturuki na Ugiriki pia anasema: "Mbali na pande mbili kuwa na tofauti kuhusiana na kisiwa cha Cyprus, pia zinatofautiana kuhusiana na suala la wakimbizi na wahajiri wa Syria." Wakati huo huo kuwepo nchini Ugiriki mamia ya wapiganaji wa Kikurdi wa PKK, mtandao uliopanuka wa harakati ya Gülen na makundi mengine ya Kikomonisti yanayopinga serikali ya Uturuki, ni mambo mengine yanayochochea hitilafu kati ya Ankara na Athens. Pamoja na hayo, ni suala lisilo na shaka kwamba, tofauti zilizopo kati ya Ankara na Athens kuhusiana na masuala ya mashariki mwa bahari ya Mediterrania na kunufaika na vyanzo vya mafuta na gesi vya bahari hiyo, ni mambo ambayo yatachochea tu mizozo ya mataifa hayo. Alaa kullihal, sambamba na kuwepo tofauti na pandashuka zote hizo katika mahusiano ya Uturuki na Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala la wahajiri, ni wazi kuwa, EU inafanya juhudi za kuzuia kujikariri mzozo wa wahajiri kama ule wa mwaka 2015 na 2016 katika eneo hilo. Kipindi hicho zaidi ya wahajiri na wakimbizi milioni moja kutoka Uturuki na kupitia nchi za ukanda wa Balkan, waliweza kuingia Ulaya na kupelekea kuongezeka pakubwa gharama za mfumo wa maisha na usalama wa umoja huo.

Tags

Maoni