Apr 06, 2020 06:01 UTC
  • Hitilafu za Russia na Saudia kuhusiana na bidhaa ya mafuta zaahirisha mkutano wa OPEC+

Vita vya bei ya mafuta baina ya Russia na Saudi Arabia vilivyoanza baada ya kufeli mkutano wa mwanzoni mwa mwezi Machi uliopita wa OPEC+ mjini Vienna vimesababisha kuporomoka kwa bei ya bidhaa hiyo kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika kipini cha miaka 18 iliyopita.

Kuendelea kwa hali hiyo kumeifanya Marekani iingilie kati kwa shabaha ya kukomesha vita hivyo vya bei ya mafuta. Hata hivyo bado hakuonekani mwanga katika uwanja huu. Vilevile mjadala juu ya swali kwamba, nani wa kulaumiwa kutokana na kuporomoka bei ya mafuta baina ya Saudi Arabia na Russia umepelekea kuahirishwa kikao cha dharura kilichokuwa kimepangwa kufanyika leo tarehe 6 Aprili ili kujadili suala la kupunguza uzalishaji wa bidhaa hiyo. Uamuzi wa kuahirishwa mkutano huo wa OPEC+ umechukuliwa huku Rais Donald Trump wa Marekani akiishinikiza OPEC na wazalishaji wengine wa mafuta wasio wanachama wa OPEC ikiwemo Rusia, kuchukua hatua athirifu kwa ajili ya kukabiliana na suala hilo na kuthabitisha soko la kimataifa la mafuta. 

Wiki iliyopita bei ya mafuta iliteremka na kufikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 18 iliyopita kutokana na kupungua ununuzi wa bidhaa hiyo uliotokana na mlipuko wa virusi vya corona na vilevile kushindwa OPEC na wazalishaji wengine wa bidhaa hiyo wasio wanachama wa jumuiya hiyo hususan Russia, kufikia makubaliano ya kupunguza kiwango cha uzalishaji na uuzaji wa bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa. Kuhusiana na suala hilo Rais Vladimir Putin wa Russia alisema Ijumaa iliyopita katika mkutano wa maafisa wa serikali na wakurugenzi wa makampuni makubwa ya uzalishaji  mafuta uliofanyika kwa njia ya video kwamba: Sababu ya kwanza ya kuporomoka bei ya mafuta ni athari za maambukizi ya virusi vya corona na kupungua kwa mahitaji ya bidhaa hiyo, na ya pili ni kujiondoa Saudi Arabia katika makubaliano ya kupunguza uzalishaji na kutoa tahafifu kubwa katika mauzo ya mafuta.

Putin ameilaumu Saudi Arabia kuwa ndiyo iliyosababisha kuporomoka kwa bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa

Saudi Arabia ilijibu haraka matamshi hayo ya Putin na kudai kuwa, Moscow ndiyo inayopaswa kulaumiwa kwa hali ya sasa na bei ya mafuta. 

Kwa sasa OPEC+ inafanya mazungumzo kuhusu suala la kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa asilimia kumi ya mahitaji ya kila siku ya dunia yaani mapipa milioni 10 kwa siku. Vilevile wazalishaji wa kundi hilo wanatarajia kwamba, nchi wazalishaji wa mafuta zisizo wanachama katika OPEC+ kama Marekani pia zitashiriki katika mpango huo, na tayari baadhi ya nchi hizo zimetangaza kuwa ziko tayari kutekeleza uamuzi huo.

Norway ambayo ni mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta na gesi huko magharibi mwa Ulaya imetangaza kuwa, iwapo wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani watakubaliana na suala la kupunguza uzalishaji wa bidhaa hiyo, itajadili suala la kupunguza uzalishaji wake.

Pamoja na hayo yote inaonekana kuwa, iwapo kila moja kati ya Russia na Saudi Arabia itaendelea kung’ang’ania msimamo wake wa kumtaja mwenzake kuwa ndiye wa kulaumiwa kwa hali ya sasa ya kuporomoka bei ya mafuta, basi mgogoro huo utaendelea kushuhudiwa. Suala hili litaikasirisha Washington ambayo inaamini kwamba, hali hiyo ina madhara makubwa kwa sekta ya mafuta ya Marekani. Nchi hiyo ambayo kwa sasa ndiye mzalishaji nambari moja wa mafuta duniani na inataka kuwa muuzaji mkuu wa bidhaa hiyo katika miaka ijayo, imechukua msimamo wa kindumakuwili kuhusiana na vita vya bei ya mafuta.

Trump na Bin Salman

Kwani katika upande mmoja Rais Donald Trump anaunga mkono suala la kupungua bei ya mafuta kwa maslahi ya watumiaji wa bidhaa hiyo ndani ya Marekani na hatimaye kupata kura nyingi za Wamarekani katika uchaguzi ujao wa rais uliopangwa kufanyika Novemba mwaka huu. Kwa upande mwingine Trump anaelewa kwamba, kuendelea kuporomoka kwa bei ya mafuta kutakuwa na madhara makubwa kwa makampuni ya bidhaa hiyo ya Marekani na yumkini ikawa sababu ya kufilisika makampuni hayo. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana akawasiliana kwa njia ya simu na viongozi wa Russia na Saudi Arabia akiomba kukomeshwa vita vya bei ya mafuta baina ya nchi hizo mbili.

Tags

Maoni