Apr 07, 2020 08:13 UTC
  • Kuongezeka wasiwasi wa kusambaratika Umoja wa Ulaya

Kuenea virusi vya corona au kwa jina la kitaalamu COVID-19, na uhaba wa vifaa vya afya na tiba barani Ulaya, kumewapelekea wataalamu na viongozi wengi wa bara hilo kuwa na wasi wasi mkubwa wa kuhatarishwa umoja na mshikamano wa Umoja wa Ulaya.

Huku akiashiria kuwa mapambano dhidi ya virusi vya corona katika mazingira ya sasa yanahitaji kuwepo umoja na mshikamano kamili wa nchi za Umoja wa Ulaya, Pedro Sanchez, Waziri Mkuu wa Hispania amesema: Inaonekana katika kuendelea vita  dhidi ya corona, mustakbali wa Umoja wa Ulaya unakabiliwa na hatari; ima tutasimama pamoja dhidi ya changamoto hii au tusambaratike kama umoja.

Onyo hilo la Sanchez limetolewa katika hali ambayo virusi vya corona vinaenea kwa kasi kubwa katika nchi za Ulaya na kuzipelekea kuchukua maamuzi yanayokwenda kinyume na kanuni na misingi ya Umoja wa Ulaya, kwa kutokuwa tayari kukabiliana na maradhi hayo pamoja na kutokuwepo vifaa vya kutosha vya kiafya na kitiba kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo. Kutekelezwa sheria za karantini, kufungwa mipaka, kutotengwa bajeti maalumu ya kukabiliana na virusi vya corona na pia kutokuwepo ushirikiano wa kutosha kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya katika kudhamini vifaa vinavyohitajika kwa madhumuni ya kukabiliana na maradhi hayo na hasa kwa nchi kama vile Italia na Hispania ambazo zinakabiliwa na tatizo kubwa zaidi la virusi hivyo, ni mambo ambayo yanahatarisha mshikamano wa umoja huo.

Pedro Sanchez, Waziri Mkuu wa Hispania

Baada ya kuenea pakubwa virusi vya corona barani Ulaya, nchi za Ujerumani na Ufaransa zimepiga marufuku mauzo ya bidhaa za afya na tiba kama vile maski na mitambo ya kusaidia wagonjwa kupumua, nje ya mipaka ya nchi hizo na hii ni katika hali ambayo Italia tayari ilikuwa imetoa ombi la kuuziwa bidhaa hizo muhimu za kuokolea maisha. Hali hiyo imezipelekea nchi kama Russia na China kutangaza kuwa tayari kushirikiana na Italia katika uwanja huo, jambo ambalo limewakasirisha sana viongozi wa Italia na kuwapelekea kukosoa vikali utendaji wa Umoja wa Ulaya. Kwa mtazamo wao, umoja huo umeshindwa kutekeleza misingi na malengo ya kuasisiwa kwake, yaani kuwepo ushirikiano kati ya nchi wanachama, na kuamua kuitenga nchi hiyo katika hali hii ngumu ya kupambana na maradhi ya corona.

Mbali na mazingira ya sasa, kuna wasiwasi pia kuhusiana na mustakbali wa umoja huo. Suala la misaada ya kiuchumi na kufidia hasara za kiuchumi zilizopatikana baada ya kumalizika janga la corona ni miongoni mwa masuala muhimu yanayowashughulisha viongozi wengi wa Ulaya kwa sasa. Kwa mtazamo wao, utendaji wa sasa wa nchi zenye nguvu zaidi katika Umoja wa Ulaya kama vile Ujerumani na Ufaransa unayaandalia uwanja makundi ya chuki na yenye misimamo ya kupindukia mipaka barani humo, kueneza fikra zao za kutaka kuzitenga nchi nyingine za Umoja huo kama Italia na Hispania, jambo ambalo bila shaka ni hatari kubwa kwa umoja huo.

Ni kwa kuzingatia hatari hiyo ndipo Yoshka Fisher na Sigmar Gabriel, mawaziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ujerumani wakatahadharisha juu ya uwezekano wa kudhoofika Umoja wa Ulaya na kutumiwa vibaya suala hilo na makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia barani Ulaya kwa ajili ya kufikia malengo yao maovu kwa madhara ya mshikamano na ushirikiano wa Umoja wa Ulaya. Kwa msingi huo wanasiasa hao wenye uzoefu mkubwa, wameitaka serikali ya Ujerumani kuandaa mpango wa kusaidia kukabiliana na mgogoro wa corona katika nchi za Italia na Hispania.

Katika uwanja huo, Jacques Delors, mkuu wa zamani wa Kamisheni ya Ulaya ametahadharisha kwa kusema: Mazingira yanayotawala sasa katika uhusiano wa viongozi wa nchi za Ulaya na kutokuwepo mshikamano kati yao yanaweza kuwa hatari kubwa kwa Umoja wa Ulaya na mustkabali wa umoja huo.

Waathirika wa Corona nchini Italia

Kabla ya mgogoro wa corona, nchi hizo pia zilikuwa zinakabiliwa na migogoro mingine mikubwa kuhusiana na masuala ya wahajiri haramu, kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya yaani Brexit na taathiza zake za kiuchumi pamoja na mdororo wa uchumi na ukosefu wa ajira barani Ulaya. Hivi sasa kuendelea mgogoro wa corona na kufungwa viwanda vingi vya uzalishaji katika bara hilo kumezidisha matatizo ya nchi hizo. Hata kama viongozi wa Ulaya wanazungumzia misaada ya kiuchumi na kusamehewa madeni ya kiuchumi baadhi ya nchi wanachama, lakini kwa mtazamo wa nchi kama vile Italia na Hispania, ahadi zilizotolewa katika uwanja huo hazitoshi na wala hakuna dhamani yoyote ya kuzitekeleza.

Waziri Mkuu wa Hispania amesema: Mshikamano wa Ulaya unapasa kutoa dhamani kwamba hakutakuwepo na pengo lolote kati ya nchi za kaskazini na kusini mwa bara la Ulaya na kuwa hakuna yoyote atakayeachwa nyuma. Katika zama hizi zenye changamoto nyingi, maamuzi muhimu yanapaswa kuchukuliwa ili kutowakatisha tamaa mamilioni ya watu wanaothamini Umoja wa Ulaya.

Ni wazi kuwa mgogoro wa hivi sasa wa corona, ambao unatajwa kuwa mgogoro mkubwa zaidi baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ni mtihani mkubwa kwa viongozi wa Ulaya kuona iwapo watasimama imara na kushikamana na thamani na misingi ya kubuniwa Umoja wa Ulaya au watahitilafiana na kupelekea kusambaratika umoja huo.

Tags

Maoni