Apr 07, 2020 14:57 UTC
  • Raia weusi wanaathiriwa kwa wingi na corona Marekani huku UN ikionya kuhusu ubaguzi katika utoaji huduma

Takwimu za majimbo mbali mbali nchini Marekani zinaonyesha kuwa jamii za raia weusi wenye asili ya Afrika ndizo zinazoathiriwa kwa wingi na maambukizo ya virusi vya corona.

Wakati Wamarekani weusi wanaunda asilimia 14.6 tu ya watu wote katika jimbo la Illinois, Shirika la Afya ya Jamii la jimbo hilo linasema, asilimia 30 ya walioambukizwa COVID-19 na asilimia 40 ya waliofariki hadi sasa ni raia weusi, hali inayoonyesha kuwa Wamarekani wenye asili ya Afrika ndio walio katika hatari kubwa zaidi ya kupoteza maisha kutokana na kirusi hicho.

Hali hiyo inashuhudiwa pia katika takwimu za majimbo ya Michigan, Louisiana na Wisconsin kati ya mengine.

Takwimu hizo zinatolewa katika hali ambayo, Kikosi Kazi cha waatalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watu wenye asili ya Afrika, kimetaka kuwepo na uwiano na usawa wa makundi mbalimbali ya binadamu wakati wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, la sivyo utoaji wa huduma kwa misingi ya rangi unaweza kusababisha vifo zaidi.

Wito huo umo kwenye taarifa iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi na wataalamu hao wanaoshughulikia haki za watu walio na asili ya Afrika, ikisema kuwa ubaguzi wa kimfumo katika utoaji  huduma unaleta matokeo ya kibaguzi na vifo zaidi na idadi ya wagonjwa miongoni mwa watu wenye asili ya Afrika.

Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho Ahmed Reid amesema, “licha ya hatua mujarabu zilizochukuliwa, serikali bado hazijatambua athari mahsusi za kiafya zinazokabili watu wenye asili ya Kiafrika au jinsi ubaguzi wa rangi na upendeleo kwa misingi ya rangi vinaweza kuchochea sera hiyo.”

Takwimu za karibuni kabisa zinaonyesha kuwa hadi sasa watu zaidi ya milioni moja na laki tatu wameshaambukizwa virusi vya corona duniani kote huku vifo vinavyotokana na COVID-19 vikipindukia 76,500.../

Tags

Maoni